Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Zambia, Inspekta Jenerali Lemmy Kajoba amekemea tabia ya baadhi ya watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuchapisha lugha zisizo na staha, matusi na maneno ya kashfa dhidi ya Viongozi wa Serikali na raia wasio na hatia.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya Habari, Inspekta Jenerali Kajoba amesema watu hao wanatakiwa kutambua matumizi ya lugha ya matusi na kashfa kwa Rais ni makosa yaliyopigwa marufuku katika kanuni ya adhabu sura ya 87 ya sheria za Zambia.
“Haya ni makosa makubwa sana, matumizi ya lugha za matusi, lugha zisizo na staha na kashfa kwa Rais ni makosa yaliyopigwa marufuku katika kanuni ya adhabu sura ya 87 ya sheria ya nchi yetu ya Zambia,” amesema Jenerali Kajoba.
Kajoba pia amewakumbusha wananchi juu ya matumizi ya mawasiliano ya kielektroniki kwa nia ya kulazimisha, kutisha, kumnyanyasa, au kumsababishia mtu msongo wa mawazo, kuwa ni kosa ambalo ni kinyume na kifungu cha 69 cha Sheria ya usalama mtandaoni na makosa ya mtandao namba 2 ya mwaka 2021.
“Katiba ya Zambia chini ya ibara ya 193 (2), inaamuru Jeshi la Polisi la Zambia kulinda amani, kudumisha sheria, utulivu, kuhakikisha usalama na usalama wa watu na kuzingatia haki za kimsingi za wananchi, sasa Polisi itawakamata na kuwashughulikia vikali wahusika wote wa makosa hayo,” amesisitiza.
Aidha, Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi la Zambia amesema Polisi wana uwezo wa kuwatafuta wahalifu katika sehemu yoyote ya nchi, mradi tu watu hao watakuwa wametumia kifaa chochote cha kielektroniki kama simu, kompyuta au kamera.
Kufuatia kauli hiyo, baadhi ya Wananchi wa Zambia wakatoa maoni yao kwa Jeshi hilo kwa kusema Polisi inatakiwa kushughulikia masuala yanayowagusa wananchi wengi kwa mara moja badala ya kuhangaika na maneno ya watu wa mitandaoni.
Katika chapisho lake mtandaoni mmoja wa wananchi wa Zambia Moses M’membe amesema, matukio kama uvunjaji wa nyumba nyakati za usiku, unyanyasaji wa kijinsia na uvunjwaji wa sheria za haki yanapaswa kupewa kipaumbele.
“Kuna hili suala la vibaka na suala la ubaguzi wa ushughulikiaji wa matukio umeenea sana kwamba wananchi wasio na hatia hawawezi kufurahia nyakati zao kwa kuhofia kukosa haki hata wanapoonewa Polisi nao wajitathmini,” alisema M’membe.
Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Lemmy Kajoba aliteuliwa kushika wadhifa huo na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema Agosti 29, 2021, na amewahi kuwa Kamishna Ofisi ya Polisi Mkoa wa Muchinga uliopo nchini humo.