Jumla ya watu 23 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya utapeli kwa njia ya mtandao.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema watuhumiwa waliokamatwa ni wale waliokuwa wakijifanya Wakuu wa Shule, Waganga wa kienyeji, ndugu wa waathirika, wahudumu wa Makampuni ya Simu au Mawakala wa Freemason.
Amesema, kukamatwa kwa watu hao kunafuatia oparesheni maalum iliyofanywa na Polisi wa kanda maalum kwa kushirikiana na timu maalumu ya Kuzuia na Kupambana na Uhalifu wa Mtandaoni, iliyofanyika kati ya Mei 18 hadi Juni 26 katika maeneo mbalimbali ya jiji ikiwemo na mtuhumiwa mmoja wa Mkoa wa Morogoro.
“Watuhumiwa hawa huwatumia watu ujumbe mbalimbali kupitia namba tofauti za simu na kujifanya wanania ya kusaidia watu kwa kuwatibia au kuwafahamu watu wanaotibu hivyo kuwashawishi wawasiliane nao badala yake huwaibia,” amesema.
Waliokamatwa ni Julius Simon Mwabula (20), mkazi wa Ifakara Mkoani Morogoro na watu wengine 22, ambapo wamekutwa na vifaa mbalimbali wanavyovitumia kufanya uhalifu ikiwemo kadi zaidi ya 50 za simu za mitandao mbalimbali, Kompyuta mpakato 2, simu 28 za aina tofauti, flash 2, modem ya mitandao yote na kompyuta ya mezani moja.