Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Songwe, ACP Gallus Hyera amewataka Waandishi wa Habari Mkoani Songwe kuripoti changamoto za kiusalama wanazokutana nazo, wakati wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Akizungumza kwenye mdahalo wa majadiliano kati ya Jeshi la Polisi mkoani humo na Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania – UTPC, Hyera amesema tasnia ya Waandishi wa Habari ina mchango mkubwa kwenye jamii na Taifa hasa katika kuibua, kuelimisha, kuburudisha, kuhabarisha masuala mbalimbali na kujenga uelewa miongoni mwa wanajamii.
Kuhusu weledi amesema, Waandishi wa Wabari wanapaswa kufanya mizania ya habari wanazozitafuta kabla ya kuzisambaza, ili taarifa au habari wanayoipata iwe imezingatia maadili ya kihabari, kitaaluma, weledi na ubobezi na si upotoshaji.
Hata hivyo, Hyera pia alitoa wito kupitia mdahalo huo kuwa endapo Mwanahabari yeyote akipata changamoto au msuguano baina yake na Askari Polisi wakati anatekeleza majukumu yake wasisite kutoa taarifa kwa uongozi wa Jeshi la Polisi, ili hatua mahususi ziweze kuchukuliwa.