Jeshi la Polisi, limetoa elimu kwa Wananchi juu ya matumizi sahihi ya fedha wanazopata Wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF, zinazotolewa kwa lengo la kusaidia kaya masikini kujiinua kiuchumi.
Mkaguzi Kata wa Kata ya Makuro ambaye ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Balumu Saguda ameyasema hayo wakati alipokuwa akiwaeleza elimu ya ushirikishwaji wa jamii kwa wanufaika wa mfuko huo katika Kijiji cha Mgong’ompoku, kilichopo Tarafa ya Mtinko, Wilaya na Mkoa wa Singida.
Amesema, wanufaika wanatakiwa kuhakikisha wanatumia vyema fedha hizo kwa kuiangalia kesho yao, ikiwemo kubuni miradi midogo midogo itakayowasaidia kuendelea kupata faida ikiwemo kilimo cha mbogamboga, biashara ndogondogo, ufugaji bora wa Wanyama kama Mbuzi, Kondoo, Kuku na Bata.
Balumu ameongeza kuwa wanufaika hao pia wajitahidi kutumia fedha wanazopewa au faida ya fedha hizo kuwanunulia watoto mahitaji ya msingi zikiwemo sare za shule, madaftari, kalamu na mabegi ya shule, huku pia akiwaelimisha jinsi ya kutoa taarifa za uhalifu na wahilifu kwa Jeshi la Polisi.