Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP David Misime amesema Askari Polisi wanapotekeleza majukumu yao wameruhusiwa kisheria kubeba silaha, ili waweze kulinda maisha ya watu na mali zao, maisha yao, mali za Serikali pamoja na silaha aliyobeba.
Misime ameyasema hayo kupitia taarifa ilitotolewa na Jeshi la Polisi, kuhusu mtindo uliojitokeza wa baadhi ya watu wanaovunja sheria na wakati mwingine kutenda uhalifu wa kujichukulia sheria mkononi pamoja na kuwashambulia Askari waliobeba silaha.
Amesema, Jeshi la Polisi nchini linawataka watu wenye tabia kama hizo kuacha mara moja kwani Askari ni binadamu kama wengine na sheria inamruhusu kutumia silaha hiyo kulinda uhai wake, wa mtu mwingine, mali za watu na za Serikali.
Aidha, SACP Misime pia amesema wale ambao wamewahi kufanya matukio kama hayo wafahamu kuwa ni lazima watakamatwa na kufikishwa Mahakamani kwani watakuwa wametenda uhalifu.