Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amemtetea kwa nguvu zote Rais Donald Trump kuhusu sera yake ya kigeni, wakati mwanadiplomasia huyo alipohojiwa na kamati ya mambo ya Nje ya Seneti.

Hayo yamejiri huku Maseneta kutoka vyama vya Republican na Democratic wakiendelea kumkosoa Rais Trump  hususani kwa matamshi yake ya hivi karibuni aliyoyatoa wakati wa mkutano wa kilele kati yake na rais Vladimir Putin wa Urusi.

Kamati hiyo ilimbana Mike Pompeo ikisisitiza kupata taarifa juu ya kipi kilichojadiliwa kati ya Trump na Putin wakati viongozi hao walipokuwa peke yao isipokuwa wakalimani kwa karibu masaa mawili.

Aidha, Pompeo amesisitiza kuwa rais ana haki ya kufanya mikutano ya faragha na kuongeza kuwa hata hivyo ana fahamu vyema kuhusiana na kile kilichojadiliwa wakati huo na viongozi hao wawili.

Hata hivyo, Seneta Bob Corker ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo ya mambo ya nje amemueleza Pompeo kuwa maseneta wana mashaka na utendaji kazi wa Ikulu ya Marekani ikiwa ni pamoja na hatua  zinazohusiana na sera za nje za nchi hiyo.

 

 

Picha: Miss Ilala, Dar24 Media wafanya ziara mashuleni
Andre Schuerrle arejea London, aahidi mazito