Rais wa Shirikisho la soka nchini TFF , Jamal Malinzi ameuandikia barua uongozi wa Lipuli ya Iringa kwa mafanikio ya kupanda daraja msimu huu kutoka Ligi Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2017/18.
Lipuli ya Iringa imepanda daraja baada ya kupita miaka 17 na Rais Malinzi amesema katika barua yake hiyo kwenda kwa Katibu Mkuu wa Lipuli, akisema: “Nitumie fursa hii kukupongeza wewe, uongozi wa klabu yako, benchi la ufundi na wadau wote wa timu ya Lipuli kufuatia kupanda daraja kwenda Ligi Kuu.
“Bila shaka ni kazi kubwa imefanyika ikihusisha kujitolea kwa ari na mali kuhakikisha mnafika hapa mlipo,” ilisema barua hiyo na kuongeza: “Rai yangu kwenu ni kuongeza juhudi na kuendesha klabu kwa weledi mkubwa zaidi ili muweze kuwa washindani wa kweli katika ligi.”
Lipuli iliyokuwa kundi “A” imepanda daraja na kuzipiku timu za Kiluvya United ya Pwani, Pamba ya Mwanza, African Sports ya Tanga, Polisi Dar, Ashanti United, Friends Rangers, Mshikamano za Dar es Salaam.