Mabingwa wa Soka nchini Zambia Power Dynamo watakitest kikosi cha Simba SC mara baada ya kurejea Tanzania kikitokea nchini Uturuki kilipoweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa 2023/24.
Miamba hiyo itakutana katika mchezo wa kuhitimisha shehere za Simba Day zitakazofanyika jijini Dar es salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumapili (Agosti 06).
Akizungumza na Waandishi wa Habari mapema leo Jumanne (Julai 25) jijini Dar es salaam, Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema mipango na maandalizi ya kuelekea Simba Day imeshaanza.
“Unyama Mwingi ni usajili mzuri, tamasha kubwa, kutimiza malengo ambayo tumejiwekea ya kuchukua mataji yote ya ndani na kufanya vizuri kimataifa.”
“Wiki ya Simba itazinduliwa tarehe 29, Julai – tarehe 6 ya mwezi Agosti. Matukio ni kama kuchangia damu, shughuliza kijamii kufanya usafi kwenye hospitali, masoko lakini pia tutakuwa na siku maalumu ya kutembelea mashujaa wa Simba.”
“Uzinduzi wa Simba Week tutafanya eneo la Buza Kanisani. Itakuwa tarehe 1, Agosti na tutaanza saa 4 asubuhi. Tunataka kufanya uzinduzi mkubwa na wa kihistoria. Wanasimba mjiandae.”
“Simba Day tutacheza na bingwa kutoka Zambia, timu ya Power Dynamos. Huyu ndio tutacheza nae kwenye kilele cha Simba Week.”
“Kwa upande wa wasanii watoto wa nyumbani, Tunda Man, Meja Kunta na Whozu watakuwepo. Siku zinapokwenda tutaendelea kutangaza wasanii wengine ambao watakuwepo.” Amesema Ahmed Ahmed Ally.
Katika hatua nyingine Ahmed Ally ametangaza vingilio katika Tamasha la Simba Day ambalo litachagizwa na shughuli mbalimbali za burudani kabla ya mchezo huo wa Kimataifa wa Kirafiki.
“Kwa upande wa viingilio, sisi kama klabu tunahitaji fedha lakini kwenye tamasha tunahitaji zaidi mashabiki, Wanasimba waje zaidi ndio maana tunawatafuta wadhamini kama CRDB ili walete fedha. Tunajali zaidi maslahi ya Wanasimba.”
“Viingilio vya Simba Day ni Platinum – Tsh. 200,000, VIP A – Tsh. 40,000, VIP B – Tsh. 30,000, VIP C – Tsh. 20000, Machungwa – Tsh. 10,000 na Mzunguko – Tsh. 5,000.”
“Kispika kinarudi mtaani kuwaita Wanasimba kwenye Simba Day. Tunaenda kuwaonyesha kwamba Uwanja wa Mkapa ni mdogo sana kwa Simba kuujaza.
“Waliopandisha kibegi kwenye Mlima Kilimanajaro, watu wote tisa tutawaalika kwenye Simba Day na watapata nafasi ya kutambuliwa na mashabiki kwenye siku ya tamasha letu.”
“Kikosi kitarejea kutoka Uturuki tarehe 1 ya mwezi Agosti.”- Ahmed Ally.