Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imezitaka taasisi za umma 361 zilizovunja sheria ya manunuzi ya umma kwa kutowasilisha kwenye Mamlaka hiyo Mipango yao ya Manunuzi ya Mwaka (GPN) kwa mwaka huu wa fedha (2016/17), kuzingatia sheria kabla hawajachukuliwa hatua stahiki.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Dkt. Matern Lumbanga amesema kuwa Kanuni ya 70 ya Kanuni za Manunuzi ya Umma za Mwaka 2013 inaitaka taasisi nunuzi kuandaa na kuwasilisha PPRA mpango wa manunuzi wa mwaka ndani ya siku 14 baada ya kumalizika kwa mchakato wa bajeti, lakini hadi sasa ni taasisi za umma 145 tu katiya 506 zilizopo (sawa na asilimia 28.6) zilizozingatia sheria kwa kuwasilisha GPN za Mwaka wa Fedha 2016/17. Lakini, hadi leo tayari siku 27 zimepita tangu kuanza kwa mwaka huo wa fedha.

Alisema sheria inazitaka kuwasilisha GPN zao  mmoja kabla ya kuanza michakato ya zabuni kwenye bajeti ya mwaka husika wa fedha, lakini hadi sasa michakato imeanza kwenye taasisi hizo bila kuwasilisha GPN.

Mwenyekiti huyo wa Bodi alisema kuwa ingawa PPRA imefanya jitihada za kuwatumia ujumbe mfupi wa simu wakuu wa vitengo vya manunuzi vya taasisi zote nchini, kuwatumia barua pamoja na kuchapisha mara kadhaa matangazo ya kuwakumbusha kuwasilisha GPN zao, bado hawajafanya hivyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Dk. Matern Lumbanga na Afisa Mtendaji Mkuu, Dkt. Laurent Shirima wakizungumza na waandishi wa habari

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Dk. Matern Lumbanga na Afisa Mtendaji Mkuu, Dkt. Laurent Shirima wakizungumza na waandishi wa habari

Alisema kuwa kutowasilisha PPRA Mpango huo wa Mwaka wa Manunuzi huchangia kuondoa uwazi na ushindani katika michakato ya manunuzi ya umma inayotumia zabuni na kwamba kaguzi zimebaini kuwepo ‘madudu’ zaidi kwenye manunuzi yaliyofanywa nje ya mpango wa manunuzi.

Aidha, Dkt. Lumbanga alisema kuwa manunuzi ambayo hayako kwenye mpango wa manunuzi wa taasisi mara nyingi hutumika kama kichaka cha rushwa na ufifishaji wa utekelezaji wa jukumu la PPRA la kusimamia manunuzi. Hivyo, hupelekea upotevu wa fedha za umma.

“Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2014/15 ilibainisha kwamba manunuzi ya shilingi bilioni 8.5 hayakuwa yamejumuishwa kwenye mpango wa manunuzi,” alisema Dkt. Lumbanga.

Alisisitiza kuwa PPRA inazo taarifa zote za taasisi ambazo hazijawasilisha mpango wa manunuzi wa mwaka uliopita na kwamba inashirikiana na Mamlaka nyingine kwa ajili ya kuzichukulia hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Dkt. Laurent Shirima alisema kuwa kitendo cha kutowasilisha PPRA mpango wa Manunuzi kwa ajili ya kuchapisha kwenye Tanzania Procurement Journal na tovuti ya Mamlaka hiyo, huwanyima fursa wananchi kujua fedha zao zitatumikaje kwenye taasisi husika ndani ya mwaka huo.

Aliongeza kuwa pia kutowasilisha GPN hizo, wazabuni hukosa fursa ya kujipanga kushiriki zabuni zilizo kwenye mpango wa manunuzi wa taasisi husika, hali inayopunguza ushindani na uwazi na kupelekea kutopatikana kwa thamani ya fedha kwenye manunuzi hayo.

Katika hatua nyingine, PPRA imezitaka taasisi nunuzi kutochapisha Mipango hiyo ya Manunuzi ya Mwaka (GPN) kwenye magazeti bila kuwasilisha kwenye Mamlaka hiyo, huku ikieleza kuwa kitendo hicho pia ni uharibifu wa fedha za umma kwani Tanzania Procurement Journal ndiyo yenye nguvu ya kisheria ya kuchapisha GPN za taasisi zote.

“Lengo la sheria hii ni kuweka One Stop Centre ya GPN zote, kuliko kuzisambaza kwenye magazeti mbalimbali, wengine hawataziona. Lakini pia kuondoa matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za umma,” alisema Dkt. Lumbaga.

BreakingNews: Mahakama Yatoa Hukumu Mauaji Ya Mwangosi
VIDEO: SAUTI ZETU WITH BERTHA PETER