Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) na Bohari ya Dawa (MSD) zimeahidi kushirikiana katika kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana kwenye ununuzi wa dawa na vifaa tiba.

Hatua hiyo imefikiwa hivi karibuni wakati Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA Bw. Eliakim Maswi alipomtembelea Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Bw. Mavere A.Tukai ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya kuboresha Ili kuhakikisha  dawa na vifaa tiba zinapatikana kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa bei nafuu.

“Lazima Taasisi hizi mbili zishirikiane kuisaidia Serikali kuokoa fedha zinapotea kwenye ununuzi wa dawa. Hii itaenda sambamba na uboreshaji wa baadhi ya taratibu zetu pamoja na mifumo,” alisema Bw. Maswi.

Bw. Maswi alieleza pia kuhusu mipango wa Serikali kuweka bei elekezi kwa bidhaa zinazonunuliwa na Serikali ikiwemo dawa na vifaa tiba, akieleza kuwa kazi inaendelea kuhakikisha bei hizo zitawekwa kwenye mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa Njia Mtandao (TANePS).

Kwa upande wake Bw. Tukai alisema kwa sasa Taasisi yake inaboresha mifumo ya ndani ikiwa ni pamoja na kukiimarisha Kitengo Cha Usimamizi wa Ununuzi (PMU) ili kiwe na Uwezo kufanya utafiti wa bei za dawa na vifaa tiba katika soko la kimataifa, jambo ambalo alisema litaiwezesha MSD kununua dawa kwa gharama nafuu kuliko ilivyo sasa.

“Kitengo chetu Cha Ununuzi tunakipandisha hadhi na Mkurugenzi na moja ya majukumu tutakayowapa ni kufanya utafiti na uchambuzi wa bei ya dawa na vifaa tiba katika  soko la kimataifa na kupendekeza namna au utaratibu bora  wa kununua bidhaa hizo,” alisema Bw. Tukai.

Bw. Tukai alieleza kufurahishwa na uamuzi wa Serikali kuweka ukomo wa bei kwa bidhaa zinazonunuliwa kupitia Mfumo wa Ununuzi kwa Njia ya Mtandao (TANePS), na kueleza kuwa ni muhimu wadau washirikishwe katika kupanga bei ili kuongeza tija kwenye utaratibu huo.

MSD ni kati ya taasisi za Serikali zinazotajwa kwenye Ripoti za PPRA kuwa na ununuzi wenye thamani kubwa zaidi kwa mwaka (big spenders), ambayo ni kuanzia Sh. 20 bilioni au zaidi.

PPRA huzijengea uwezo taasisi za umma kwa kutoa mafunzo ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na jinsi ya kutumia TANePS, pamoja na kutoa miongozo mbalimbali ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana kwenye Ununuzi huo.

Serengeti Girls kundi moja na Ufaransa
Makumbusho ya wapigania Uhuru nchini kuboreshwa