Mafunzo ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na matumizi ya Mfumo wa Ununuzi kwa Njia ya Mtandao (TANePS) yanayotolewa na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) yameboresha utekelezaji wa miradi katika Mkoa wa Morogoro.
Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Mkoa huyo, Mhandisi Emmanuel Kalobelo alipozungumza na wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka PPRA waliomtembelea ofisini kwake wiki hii.
Mhandisi Kalobelo amesema kuwa ameshuhudia mabadiliko makubwa chanya katika michakato ya zabuni baada ya watendaji wa taasisi za mkoa huo kuhudhuria mafunzo hayo, hatua ambayo imesaidia kuongeza upatikanaji wa thamani ya fedha kwenye ununuzi wa umma.
“Kwakweli awali tulikuwa nyuma sana, lakini baada ya kupata mafunzo na kuanza kutumia TANePS sasa hivi tuko vizuri sana na miradi yetu mingi inaenda vizuri sana,” Mhandisi Kalobelo alisema.
“TANePS imepunguza gharama za makaratasi na vikao vingi. Pia, ile kuonana moja kwa moja na wazabuni kwenye hatua za mwanzo za michakato nayo ilikuwa inaongeza mianya ya rushwa na udanganyifu kwa wasio waadilifu. Lakini sasa hivi mfumo haudanganyi, wote wana fursa sawa. Na hata waki-bid wanaweka gharama ndogo ya sokoni kwakuwa hawajui nini kiko ndani ya zabuni kwenye mfumo,” aliongeza.
Aidha, Katibu Tawala huyo aliishukuru Serikali kwa kuanzisha TANePS na kutoa wito kwa taasisi nunuzi kuhakikisha watendaji wake wanashiriki kikamilifu kwenye mafunzo na kutumia elimu wanayoipata kuhakikisha kila zabuni inapitia mfumo huo kama Serikali ilivyoelekeza.
Ameishukuru pia PPRA kwa kuendelea kutoa mafunzo hayo kadri inavyowezeka, kwakuwa ukidhi wa sheria unapoongezeka miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa gharama inayoendana na mradi husika.
Naye Meneja wa Miongozo ya Ununuzi kutoka PPRA, Bw. Castor Komba, alimshukuruhy Katibu Tawala huyo kwa mrejesho huo na kumuomba kama mdau kuzikumbusha taasisi nunuzi zilizo chini yake kuendelea kuwawezesha watendaji kuhudhuria mafunzo hayo.
“Mamlaka inaendelea kuweka nguvu zaidi kwenye mafunzo kwakuwa ni jukumu lake muhimu lakini pia uzoefu unaonesha kadri watendaji wanavyozidi kupewa mafunzo, kiwango cha ukidhi wa sheria kinapanda angalau kila mwaka,” alisema Bw. Komba.
“Hii maana yake ni kwamba watendaji wenye elimu na waadilifu wanaongeza tija kwenye jitihada za Serikali yetu ya Tanzania katika kuwaletea maendeleo wananchi kupitia miradi mikubwa na midogo inayoakisi thamani halisi ya fedha iliyotumika,” aliongeza.
PPRA imefanya mafunzo ya siku nne, kuanzia Februari 23-26, 2021 mjini Morogoro, kwa watendaji takribani 50 wa taasisi mbalimbali za Serikali.