Watu zaidi ya 30 wanaaminika kupoteza maisha kutokana na kupata shinikizo la damu kufuatia nyumba zao kubomolewa katika bonde la mto Mkwajuni jijini Dar es Salaam.

Pamoja na idadi hiyo ya vifo, watu kadhaa pia wameripotiwa kulazwa katika hospitali mbalimbali jijini Dar es Salaam kutokana na shinikizo (presha) walilolipata kutokana na zoezi la bomoabomoa linaloendelea, iliyoanza mwishoni mwa mwaka jana.

Diwani wa Kata ya Hananasif, Ray Kimbita alithibitisha kutokea kwa idadi kubwa ya vifo kutokana na zoezi hilo huku akieleza kuwa wamepanga kukutana Januari 15 mwaka huu ili wakazi wa maeneo hayo waweze kufanya ibada maalum ya pamoja ya kuwaombea marehemu.

Baadhi ya majina ya waliofariki katika zoezi hilo ni Joviti Hussein aliyefariki Desemba 17 mwaka jana, Angel Ally maarufu kama Mama Mzungu. Wengine ni Neema Fungo, aliyefariki Desemba 18, na Bibi Bakari Fungo (mama yake Neema).

Mmoja kati ya waathirika wa zoezi la bomoabomoa aliyelazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alieleza sababu zilizopelekea kufikishwa hospitalini hapo.

“Nyumba yangu ilikuwa kubwa kati ya nyumba zote zilizopo katika bonde la Mkwajuni, nilikuwa naikarabati mimi mwenyewe na nilikuwa bado sijahamia,” Bunda alimueleza mwandishi wa Tanzania Daima. “Ni nyumba kubwa ya vyumba nane na zilikuwa ni nyumba mbili kwa pamoja. Nilipoona nimebomolewa kwa sababu nguvu zote niliwekeza hapo ndipo nilipata mshtuko, nikapelekwa hospitali ya private ilikuwa Desemba 18, lakini nilizidiwa ndipo nikahamishiwa hapa Muhimbili Desemba 24.”

Zoezi la bomoabomoa linaendelea kwa watu waliojenga katika maeneo yaliyojengwa kinyume cha sheria katika maeneo ya mabondeni na maeneo ya wazi. Serikali imeeleza kuwa zoezi hilo ni kwa nchi nzima na kuwataka wananchi waliojenga kinyume cha sheria kujiandaa kisaikolojia.

 

Mbwana Samatta Aipaisha Tanzania
Maalim Seif Awatoa wasiwasi wazanzibari