Prince Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia amesema kuwa alimfahamu mwandishi aliyeuawa, Jamal Khashoggi kama mtu hatari na muumini wa itikadi kali, kwa mujibu wa Washington Post na New York Times.
Kauli hiyo ya Prince Mohammed imeripotiwa kuwa aliitoa baada ya kupiga simu katika Ikulu ya Marekani siku chache baada ya nchi yake kukiri kuwa Khashoggi aliuawa mwezi Oktoba ndani ya ofisi za ubalozi wake uliopo Istanbul nchini Uturuki.
Kwa mujibu wa ripoti ya Washington Post, katika mawasiliano ya simu kati ya Prince Mohammed na mshauri wa masuala ya ulinzi wa Marekani, John Bolton, Prince alisema kuwa Khashoggi alikuwa mwanafamilia wa kundi la ‘Muslim Brotherhood’ ambalo ni kundi la harakati za maguezi ya itikadi kali.
Mawasiliano hayo ya simu yanaripotiwa kufanyika Oktoba 9 mwaka huu, wiki moja baada ya Kashoggi kupotea.
Imeelezwa kuwa Prince Muhammed aliishauri Ikulu ya Marekani kuendelea kulinda uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Hata hivyo, familia ya Khashogi imesisitiza kuwa marehemu hakuwa mtu hatari kwa taifa na kwamba hakuwahi kuwa mwanafamilia wa kundi la Islamic Brotherhood.
“Jamal Khashoggi hakuwa mtu hatari kwa namna yoyote. Kudai vinginevyo ni upuuzi mtupu,” imeeleza familia yake kupitia Washington Post.
Khashoggi alikuwa mwandishi wa habari wa Washington Post na aliuawa baada ya kuingia kwenye ofisi za ubalozi wa Saudi Arabia nchini Uturuki.
Saudi Arabia imekanusha kuhusika moja kwa moja na mauaji ya Khashoggi huku ikikiri kuwa maafisa wake walitekeleza mauaji hayo kwa sababu binafsi. Nchi hiyo iliahidi kuwachukulia hatua kali watu waliohusika na mauaji hayo.
Prince Mohammed amekuwa sehemu ya lawama na tuhuma za mauaji hayo kutokana na historia ya mwandishi huyo kama mkosoaji wake mkuu.