Maandamano ya UKUTA hayawezekani kwani hii ni ndoto ya mchana na hayana msingi wowote wala tija kwa wahusika hata kwa Taifa.

Hayo yalisemwa na Muhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Benson Bana katika mahojiano maalum.

“Wanaotaka kuandamana wanajidanganya na kuwalaghai wenzao kwani kufanya operesheni ni suala la dola na si la mtu au kikundi cha watu, hivyo maandamano hayo hayawezekani kabisa, alisema Prof. Bana.

Ameongeza kuwa wanaojiita UKUTA ni kwamba Mhe. Rais John Pombe Magufuli amewanyima ajenda kwani utendaji wake umezidi fahamu zao na kuwafanya waanze kutapatapa wasijue nini la kufanya.

Prof. Bana amesema kama viongozi wa UKUTA ni waungwana inabidi watamke wazi kuwa wametafakari na kuona kuwa maandamano hayana maana hivyo wameamua kuyasitisha nchi nzima.

Kuhusu utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano, Prof. Bana alisema ni Serikali yenye maamuzi ya uhakika na inayowajali watu wote bila kujali itikadi zao za vyama, dini wala makabila hivyo inabidi watanzania waipende na kuiheshimu.

“Rais Magufuli utendaji wake ni wa kuigwa na viongozi wengi Duniani kwani anafanya maamuzi ya uhakika ikiwemo kukuza uchumi kwa kukusanya kodi na kuziba mianya ya ubadhirifu wa mali ya umma, alisema Prof. Bana.

Pamoja na kuwa Rais Magufuli amekuwa madarakani kwa kipindi kifupi, viashiria vyote vinaonyesha kuwa ni kiongozi imara na shupavu kutokana na mambo makubwa ambayo ameyafanya kwa kipindi hiki kifupi. Katika kipindi hiki kumekuwepo na nidhamu katika utumishi wa umma, kodi inakusanywa kwa kiwango kikubwa na elimu ya msingi inatolewa bure kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala inavyosema, alisema Prof. Bana.

Aidha, Prof Bana amesema kuwa wanaomlaumu Mhe. Rais ni wale ambao hawajitambui na labda wanaona mianya ya ubadhirifu anayoendelea kuiziba, wao wanakosa mapato, vinginevyo Rais anafanya vizuri katika kuliongoza Taifa.

“Rais Magufuli yuko sahihi kwa jinsi anavyosimamia vipaumbele vya Serikali ikiwemo elimu bure, kukusanya kodi na kuzuia mianya ya rushwa pia dhamira ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda, alisema Prof. Bana.

Prof. Bana ameelezwa kusikitishwa kwake na watu wanaomkosea Rais heshima na kumwita “Dikteta Uchwara.”Amesema watu hawa inabidi wazalendo wakemee kabisa vitendo vya namna hii ambavyo ni utovu wa nidhamu kwa kiongozi.

Akizungumzia uamzi wa kuhamia Dodoma, Prof. Bana alisema kuwa ni uamzi wa busara kutekeleza azma ya Serikali ya miaka takribani arobaini iliyopita. Hivyo kuhamia Dodoma kutaufanya mji huo kuendelea zaidi kimiundombinu na kiuchumi.

Aliongeza kuwa mikoa ya jirani nayo itanufaika kiuchumi kwani itakuwa karibu na makao makuu ya nchi na pia kuhama huko kutatoa fursa kwa Dar es Salaam kukua zaidi kibiashara.

Prof. Bana ameitofautisha Serikali ya Awamu ya Tano na awamu nyingine nne zilizopita kwa kutokuwa na kigugumizi katika kufanya maamuzi yake ikiwemo hii ya kuhamia Dodoma, kuondoa wabadhirifu katika utumishi wa umma na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na fedha hizo kutumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama afya, elimu na miundombinu

Idadi Ya Wagonjwa Wa Trakoma Yapungua
STDFAA Wamtaka Nape Kuharakisha Sera Ya Filamu