Ufaransa imeonesha nia ya kuisaidia Tanzania katika ukarabati wa jengo la pili la Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere ambao ulijengwa kwa mkopo kutoka Serikali ya Ufaransa pamoja na kushirikiana katika kukuza biashara, uwekezaji na masuala ya ulinzi na usalama.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulaya na mambo ya Nje wa Ufaransa Jean Yves Le Drian Jijini Paris Nchini Ufaransa ambapo katika mazungumzo hayo Ufaransa imekubali kushirikiana na Tanzania katika masuala ya maendeleo,uwekezaji na biashara ikiwa ni pamoja na kukarabati jengo la uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (terminal two).
Aidha Prof Kabudi ameongeza kuwa Ufaransa imepokea ombi la Tanzania la kupatiwa yuro milioni 718 kama msaada ama mkopo kwa ajili ya kusaidia katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo awamu ya tano ya ujenzi wa mradi wa mabasi ya mwendo kasi Jijini Dar es Salaam, Ujenzi wa Uwanja wa ndege Mwanza,miradi ya nishati ya jua na maji.
Kwa upande wake Waziri Jean Yves Le Drian amemhakikishia Prof. Kabudi kuwa Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na serikali ya Ufaransa kupitia shirika lake la maedeleo la AFD pamoja na kuwashawishi wawekezaji na wafanyabiashara wa Ufaransa kuwekeza Tanzania.
Aidha Le Drian ameipongeza Tanzania kwa kutoa mchango mkubwa katika masuala ya ulinzi na usalama na kuhamasisha amani katika ukanda wa Afrika hususani eneo la maziwa makuu pamoja na suala la kuwahifadhi wakimbuizi wanaokimbia machafuko katika nchi zao.
Katika tukio jingine Tanzania imewasilisha ombi la kutaka Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO kuanza mchakato wa kukifanya Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha za kufanyia kazi kwa shirika hilo ikiwa ni pamoja na kutenga siku maalum ya Kiswahili duniani.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, Auerey Azoulay amesema masuala ya urithi wa dunia si tu maeneo mbalimbali yaliyotengwa bali pia UNESCO inathamini urithi wa tamaduni mbalimbali ikiwemo lugha ya Kiswahili.