Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amemteua Zainab Mndolwa kuwa mkurugenzi wa fedha na uchumi, na naibu wake Omar Mohammed Omar, mkurugenzi wa mambo ya nje, Bunge na sera, Mohammed Habibu Mnyaa na naibu wake, Mohammed Ngulangwa.
Prof. Lipumba amefanya uteuzi huo wa wakurugenzi mbalimbali wa chama hicho pamoja na viongozi wa jumuiya za chama kutokana na mamlaka aliyonayo kupitia katiba ya chama, ibara ya 91(1) (f) inayomtaka kuteua kutoka miongoni mwa wajumbe wa mkutano mkuu wa Taifa, wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi na wanachama jasiri.
Wengine walioteuliwa ni mkurugenzi wa mipango na uchaguzi, Mneke Jafar na naibu wake, Mohammed Vuai Makame, mkurugenzi wa habari, uenezi na mahusiano ya umma, Abdul Kambaya na naibu wake, Mbarouk Seif Salim.
Aidha, Prof. Lipumba amenteua Haroub Mohammed kuwa mkurugenzi wa haki za binadamu na sheria, naibu wake akiwa ni Salvatory Magafu wakati Thinney Juma Mohammed akiteuliwa kuwa mkurugenzi wa mafunzo na uhamasishaji na naibu wake, Masoud Omary Mhina.
Pia, Prof. Lipumba amefanya uteuzi wa viongozi wa jumuiya za chama huku akisema viongozi hao watakaimu nafasi zao mpaka pale watakapochaguliwa kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano kwa mujibu wa katiba ya chama.
“Kwa kuzingatia hali ya jumuiya zilivyo sasa, nateua makaimu wenyeviti na makamu wenyeviti na makaimu katibu watendaji na manaibu wao katika jumuiya zote za chama watakaoratibu na kukamilisha uchaguzi wa jumuiya za chama,” amesema mwenyekiti huyo.
Walioteuliwa ni Hamidu Bobali (kaimu mwenyekiti wa jumuiya ya vijana wa Cuf – Juvicuf), makamu wake, Faki Suleiman Khatib na kaimu katibu mtendaji, Yusuph Kaiza Makame na naibu wake, Mbaraka Chilumba.
Kaimu mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Cuf (Jukecuf) ni Dhifaa Mohammed Bakar na makamu wake ni Kiza Mayeye, kaimu katibu mtendaji ni Anna Ryoba na naibu wake ni Leila Jabir Haji.
Kwa upande wa Jumuiya ya Wazee wa Cuf (Juzecuf), kaimu mwenyekiti ni Mzee Chunga na makamu wake ni Hamida Abdallah, kaimu katibu mtendaji ni Hamis Makapa na naibu wake ni Said Ali Salim.
Lipumba amefanya uteuzi huo baada ya CUF kupitia kipindi kirefu cha mgogoro ulioibua makundi mawili ya CUF Lipumba na jingine likiwa chini ya aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.