Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini, Prof. Ibrahim Lipumba amemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kurudi katika meza ya mazungumzo na kumaliza tofauti zao.
Ameyasema hayo mapema hii leo jijini Dar es salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amemtaka Katibu Mkuu huyo kurudi wafanye mazungumzo na atambue kuwa yeye ndiye Mwenyekiti wa CUF na ndiye boss wake.
“Maalim analalamika lakini malalamiko yake hayana msingi, yeye ni Katibu Mkuu anapaswa kufuata misingi ya Mwenyekiti, anatambua kuwa Mwenyekiti ni boss kwa mujibu wa Katiba ya CUF, Mwenyekiti nipo yeye aje kufanya kazi hapa,”amesema Prof. Lipumba
Amesema kuwa Maalim ni mkongwe katika siasa hivyo ni vyema kukawa na maelewano ili kazi za chama zisonge mbele katika kukiimarisha chama cha wananchi CUF ili kuweza kurudisha umoja na mshkamano waliokuwa nao.
Aidha, Prof. Lipumba amesema kuwa kama Katibu Mkuu wa CUF ataendelea na kutotimiza wajibu wake wa kufika ofisini kwa ajili ya majadiliano na mazungumzo kwa lengo la kumaliza migogoro yao basi Naibu Katibu Mkuu ataendelea kukaimu nafasi hiyo kwa mujibu wa Katiba yao ya CUF.
Hata hivyo, Lipumba amekipiga dongo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) toka kimempokea, Edward Lowassa wameacha ajenda ya ufisadi na wameiweka kando ajenda hiyo na kusema sasa hivi wao ndiyo ajenda yao hiyo