Mwenyekiti wa chama Chama cha Wananchi (CUF), anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, kesho Jumapili Januari 27, 2019 ametangaza kuwa watafanya maombi baada ya miaka 17 kupita tangu vurugu za mwaka 2001.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa imepita miaka 17 tangu zitokee vurugu hizo hivyo chama hicho kimeona kina sababu ya kuwaombea waliopoteza maisha wakati wakidai demokrasia.
“Maombi hayo ni kwa ajili ya kuwakumbuka watu waliopoteza maisha katika vurugu zilizojitokeza mwaka 2001 ikiwa ni baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2000,”amesema Profesa Lipumba
Aidha, amesema kuwa maombi hayo yatafanyika katika viwanja vya Mnyamani Buguruni jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni ambapo maombi hayo yataenda sambamba na ofisi zote za chama kupeperusha bendera nusu mlingoti.
Hata hivyo, Chama Cha Wananchi (CUF) kimekuwa na migogoro isiyokuwa na mwisho baada ya Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na msajili wa vyama vya siasa nchini, Prof. Ibrahim Lipumba kutofautiana na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad