Ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe, na kutangaza kilomita 1,500 ambazo ndio kiini cha mogoro wa Loliondo kuwa sehemu ya pori tengefu, imezua taharuki kiasi cha baraza la madiwani kutamka anawavuruga na kuingilia maagizo ya Waziri Mkuu.
“Tamko hili limeibua upya tafsiri ya mgogoro huu na kuwafanya watu na hasa sisi madiwani kuamini kuwa Waziri Prof. Maghembe, hana nia ya kumaliza mgogoro huu, utaratibu huu wa kukiuka makubaliano umekuwa ni maarufu wa mgogoro huu kwa miaka mingi sasa,”amesema Mwenyekiti wa halimashauri ya Ngorongoro, Methew Siloma.
Madiwani hao wamesema kuwa, taarifa ya Waziri Maghembe ya kutenga eneo la mgogoro kwa staili anayoitumia si tu anavuruga dhamira ya wananchi na wawekezaji kutatua mgogoro lakini pia inaingilia maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Aidha, Silomba amesema kuwa kazi ya kuratibu mjadala huo wa wadau, ulifanyika chini ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na tangu aanze imekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kufanyika kwa mijadala na wadau, ikiunganisha kati ya kamati ya jamii, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na utalii na wawekezaji.
Hata hivyo, Siloma amesema kuwa wadau husika wamelitembelea eneo la mgogoro na kuweka mkakati wa kuendelea na mjadala huo lakini tofauti na matarajio hayo wanamtuhumu Waziri Maghembe kwa kuvuruga dhamira ya wananchi na wawekezaji ya kumaliza mgogoro huo.