Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa ameagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Manga uliopo Wilaya ya Mpanda Mjini, mkoani Katavi achunguzwe na TAKUKURU kutokana na kutumia mabomba yasiyokidhi viwango.

Ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha majumuisho na uongozi wa mkoa mara baada ya kumaliza ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Katavi.

Mradi huo wa Manga wenye thamani ya Shilingi milioni 575 unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Mpanda (MUWASA) na kutekelezwa na mkandarasi anayejulikana kama Nyalinga Investment Co. Ltd, uligundulika kuwa una kasoro ya mabomba mara baada ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji mji wa Mpanda (MUWASA), Mhandisi Zacharia Nyanda kubaini ubovu wa mabomba hayo na kuyapeleka Shirika la Ubora wa Viwango Tanzania (TBS) kwa ajili ya vipimo na kuonekana hayakidhi viwango.

Amesema kuwa ripoti hiyo ya TBS imeonyesha kuwa kuna tofauti kubwa ya vipimo vya mabomba yaliyotumika na vipimo vinavyoonekana kwenye mkataba, hivyo kuthibitisha udanganyifu wa mkandarasi huyo na kumpongeza Mhandisi Nyanda kwa kugundua mapungufu hayo.

“Nataka TAKUKURU wafanye uchunguzi mkandarasi huyu alipataje kazi wakati hana uwezo, na kama kuna mtu kutoka wizarani anahusika kwa namna yoyote katika jambo hili, siku zake zinahesabika maana nitamchukulia hatua mara moja,’’amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, amesema kuwa atamripoti mkandarasi huyo kwenye Bodi ya Wakandarasi nchini (CRB) ili wamchukulie hatua na kutaka asipewe tena kazi zozote za miradi ya maji, kwa kuwa wizara yake haitaruhusu wakandarasi wasio na uwezo kuendelea kula kodi za wananchi hali wakiendelea kukosa huduma ya majisafi na salama.

Hata hivyo, ameongeza kuwa atahakikisha changamoto zote zinazokabili ujenzi wa mradi huo zinapatiwa ufumbuzi haraka ili mradi huo unaogharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 268.35 zilizotokana na mkopo nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Exim Bank unakamilika ifikapo Novemba, 2019 badala ya mwaka 2020 kulingana na mkataba

Makala: Albino wana haki ya kuishi, Tuwalinde
Mlinga: Chadema acheni kudhihaki msiba