Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya Sumitomo Mitsui anayejenga barabara ya juu (Fly over) ya Tazara kuongeza kasi ya ujenzi huo ili  kupunguza muda wa ujenzi wa mradi huo.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam katika eneo la ujenzi huo  Prof. Mbarawa amepongeza hatua iliyofikiwa sasa lakini pia amesisitiza kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo ili wananchi waweze kunufaika.

“Hakikisheni badala ya kutumia miezi 35 kujenga mradi huu, mnatumia miezi pungufu zaidi ili kuwawezesha wananchi na wadau wengine kunufaika na fursa za mradi huu”, amesema prof. Mbarawa.

Hatua hiyo itapelekea kuwezesha wananchi kunufaika na mradi huo mapema, hivyo kupunguza gharama wanazozipata kutokana na msongamano wa magari uliopo sasa jijini Dar es salaam.

Naye, Balozi wa Japan nchini Bw. Masaharu Yoshida, amemhakikishia Waziri huyo kuwa ujenzi wa mradi huo utamalizika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa, hivyo kuondoa changamoto ya msongamano katika barabara ya Nyerere na Mandela.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa miradi kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Eng. Crispinius Ako, amesema kati ya nguzo 66 zinazohitajika kwenye awamu ya kwanza ya ujenzi huo, tayari nguzo 43 zimeshasimikwa ardhini, hali itayopelekea ujenzi huo kwenda kwa kasi.

Mpaka sasa mradi huo uliozinduliwa tarehe 1 Disemba 2015 umekamilika kwa asilimia 25.3 na zaidi ya shilingi bilioni 96.5 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa mradi huo ambao utakamilika mwezi Oktoba mwaka 2018.

 

TPA Yaboresha utoaji huduma kwa wateja
Video: Yusuph Manji kitanzini tena uhamiaji