Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amempa muda wa miezi kumi Mkandarasi wa Kampuni ya CICO anayejenga barabara ya Tabora-Sikonge yenye urefu wa km 30 kwa kiwango cha lami kukamilisha kazi hiyo.

Mbarawa ameyasema hayo mkoani Tabora mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo na kuelezea kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake.

“Nakupa miezi kumi tangu sasa hadi mwezi Mei mwakani uwe umeikabidhi Serikali barabara hii”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa ukamilishaji wa barabara hiyo uendane na viwango na ubora vinavyoendana na thamani ya fedha waliyopewa ili barabara hiyo iweze kudumu kwa muda uliopangwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjiini Mwalimu Queen Mlozi, amemshukuru Prof. Mbarawa kwa kufuatilia kwa karibu mradi huo ambao utachochea kasi ya maendeleo mkoani humo.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Tabora Eng. Damian Ndabalinze, amemhakikishia Prof. Mbarawa kuwa atamsimamia mkandarasi huyo kikamilifu ili barabara hiyo ikamilike katika kipindi cha miezi kumi.

Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa amempongeza Mkandarasi CHICO anayejenga barabara ya Kaliua-Kazilambwa yenye urefu wa KM 56 iliyokamilika kwa kiwango cha lami na kusisitiza wananchi kuilinda na kuitunza barabara hiyo kwa kutoiharibu miundombinu yake.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua,  Abel Busalama, ameipongeza Serikali kwa jitahada zake za kufungua Mikoa na Wilaya nchini kwa kujenga barabara za lami kwani barabara hiyo imefungua shughuli za kiuchumi na kimaendeleo wilayani kwake.

 

JPM ashiriki ibada na kuendesha harambee ujenzi wa Kanisa Chato
Video: ADC waunga mkono kauli ya JPM kuhusu wanafunzi wanaopata mimba