Watu watatu wilayani Karagwe Mkoani Kagera wanashikiliwa na Polisi na kuhojiwa kutokana na sintofahamu ya uendeshaji wa mradi wa maji katika kata ya Nyakabanga kuhusiana na masuala ya ukusanyaji wa fedha.
Agizo la kukamatwa kwa watu hao ambao ni mwenyekiti wa kamati ya watumiaji maji wa kata hiyo, katibu pamoja na muweka hazina limetolewa na waziri wa maji Prof. Makame Mbarawa alipo utembelea mradi huo Julai 12 mwaka huu na kubaini kuwepo ubabaishaji katika uendeshaji.
Prof. Mbarawa amechukua uamuzi huo baada ya wananchi pamoja na kamati ya uendeshaji wa mradi huo kusema kuwa hawapati maji kwa uhakika na maeneo mengine kuwa hayatoki suala lililompelekea kuanza kuvizungukia baadhi ya vizimba ndipo alipogundua kuwa upo udanganyifu wa maji kuuzwa na pesa hazionekani.
“Hapa kumekuwepo na ubabaishaji katika masuala ya pesa, maji yanauzwa na pesa haionekani, mwanzoni mmedanganya kuwa maji hayatoki nikaamua kuzungukia vizimba na nikagundua maji yanatoka na mita pia zinahesabu maji yaliyotumika, sasa kutokana na hilo hawa watu watatu naondoka nao ili wakaeleze vizuri.” amesema Prof. Mbarawa
Akiwa Wilayani Kyerwa alipo utembelea mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya zaidi shilingi milioni 500, waziri Mbarawa amemtaka Mhandisi wa maji mkoa wa Kagera kuwa makini na kampuni ya DONCONSULTANT LTD ambayo alikuwa ameshaingia nayo mkataba wa miradi ya Maji wilayani humo.
Aidha, Prof. Mbarawa ameongeza kuwa mhandisi wa mkoa amekuwa akisaini mikataba mbalimbali ambayo ndani yake kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha na kupelekea miradi mingi ya maji Mkoani Kagera kushindwa kutekelezwa kwa wakati.
“Ninachotaka uelewe Mhandisi wa Mkoa ni kwamba makampuni haya yamekuwa yakipiga pesa ndefu huenda na wewe ulikuwa unajua ila sasa sitakufukuza nataka ujifunze, haiwezekani bomba la laki sita ukaandikiwa linauzwa milioni mbili na wewe ukasaini ili pesa hiyo itoke.” ameongeza Prof. Mbarawa.
Hata hivyo, baadhi ya watumiaji wa maji katika mradi wa maji wa Mabira wameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuwapatia huduma ya maji, ambayo ilikuwa kitendawili tangu Tanzania inapata uhuru na kuwataka mawaziri kuendelea kuwatembelea ili kuzijua Kero zao.