Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo amelipiga marufuku Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania kujihusisha na Gesi aina ya Helium kwani haina uwezo wa kushughulikia Gesi hiyo.
Amesema kuwa Shirika hilo linajishughulisha na mambo mengi hivyo ni bora likabaki na shughuli ambazo linazifanya kwa sasa na si kujiongezea mzigo mwingine.
Aidha, Gesi aina ya Helium iligundulika mwaka mmoja uliopita katika Bonde la Ufa, huku Mkoa wa Rukwa pekee ukiwa na hazina ya helium ya ujazo wa futi bilioni 54 (bfc) mara saba ya uhitaji wa dunia.
“TPDC haijafanya kinachohitajika katika Petroli na Gesi Asilia kiutafutaji na uzalishaji, hivyo ni bora wasijihushe kabisa na Gesi ya helium kwa sababu hawatafanikiwa, niwatake tu waendelee na shughuli zao wanazofanya kwa sasa,”amesema Prof. Muhongo.
Hata hivyo, Prof. Muhongo amesema kuwa ugunduzi wa Gesi hiyo umeiweka Tanzania katika ramani itakayoziba pengo la upungufu wa Gesi hiyo duniani iliyopo kwa sasa baada ya kuongezeka kwa matumizi yake.