Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene amemteua mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Davis Mwamfupe kuwa diwani katika Manispaa ya Dodoma.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi imeeleza kuwa Profesa Mwamfupe pamoja na wenzake wawili Roze Nitwa (CCM) na Vicent Tibalindwa (Chadema) wameteuliwa na Waziri kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo.
Kunambi amesema Waziri Simbachawene aliteua majina sita kwa vyama vya Chadema na CCM ndipo wakayapigia kura likiwamo jina la Mwamfupe aliyetokea CCM.
“Waziri alitumia sheria namba 288 (24) (2d) ya Serikali za mitaa na kanuni za uteuzi za mwaka 2010 sura ya 4 (1) na 5 (1) vinavyompa mamlaka ya kufanya hivyo bila kuulizwa na humteua mtu ambaye ni mkazi wa eneo husika,” alisema Kunambi.
Manispaa ya Dodoma haina Meya baada ya Jaffary Mwanyemba kuondolewa na madiwani Machi mwaka huu kwa madai ya matumizi mabaya ya madaraka.
Akizungumzia uteuzi huo, Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jumanne Ngede amesema baraza la madiwani halina shaka na uteuzi huo na kwamba watapewa ushirikiano katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ikiwamo mchakato wa makao makuu.
Amesema mpango uliopo katika manispaa hiyo ni kujipanga kuwa na ugeni mkubwa ambao umeingia mkoani hapo ikiwemo maofisa wa serikali.