Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 61 wa Kitanzania kwa mwaka huu.

Akizungumza katika sherehe za kuwaaga wanafunzi hao katika eneo la Ubalozi wa China Jijini Dar es Salaam, Prof. Ndalichako amesema kuwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi zote mbili kati ya Tanzania na China utakuwa ni ushirikiano endelevu.

Prof. Ndalichako ameiomba Serikali ya China kuweka utaratibu wa ufadhili kwa wakati mwingine uwe kwa wahandisi wa umeme hasa kutokana na mradi wa ujenzi wa Reli kukamilika hivi karibuni.

“Tunaomba kuwepo na ufadhili katika masuala ya usafiri kwa ujumla hasa reli kwa kutambua kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya Standard Gauge kwa hiyo tungependa kuwa na mainjinia ambao watakuja kuendesha mradi huo pindi utakapokamilika,” amesema Prof. Ndalichako

Aidha, Prof. Ndalichako amewapongeza wanafunzi waliochaguliwa kupata nafasi ya ufadhili wa masomo nchini China na kuwashauri waweze kutumia nafasi hiyo vizuri ili kuweza kupata ujuzi na maarifa ili baadaye waweze kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha wanaongeza kasi ya kujenga uchumi nchini.

“Mkawe mabalozi wazuri katika nchi yetu, mnakwenda China mtakutana na watu wa China pia mtakutana na watu wa mataifa mengine ambao wengine hawajawahi kufika nchini Tanzania kwa hiyo kielelezo chao ni matendo yenu, tabia zenu na mwenendo wenu, nawaomba sana vijana msiende kutengeneza jina baya,”ameongeza Prof. Ndalichako.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 20, 2019
Uingereza yafadhili masomo watumishi Wizara ya Fedha na Mipango