Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, Profesa Mwesiga Baregu amekosoa uamuzi wa  Serikali kuhamia Dodoma hivi sasa kwa kutumia sababu za miaka takriban 50 iliyopita.

Profesa Baregu ameoneshwa kushangazwa na jinsi ambavyo uamuzi huo umefikiwa bila kufanyika kwa tathmini, akieleza kuwa yapo mambo mengi ambayo yamebadilika na kwamba hata uamuzi uliotolewa miaka hiyo ilitokana na tathmini iliyozingatia hali halisi ya wakati huo.

“Hili suala la kuhamia Dodoma, huwezi leo hii miaka karibu 50 imepita, ukatekeleza maamuzi ya miaka ya (19)70, kwa sababu zile zile za miaka hiyo!” Profesa Baregu anakaririwa na gazeti la Nipashe.

Alisema kuwa hivi sasa nchi ina rasilimali nyingi ya kufanya utafiti na tathmini kabla ya kuchukua maamuzi hayo huku akitahadharisha kutotumia kigezo cha kutekeleza maamuzi ya Mwalimu Julius Nyerere ambayo hayakutekelezwa hadi sasa kufanya maamuzi kwa njia ileile ya zamani wakati huu.

“Tusije tukafanya madudu kwa jina la huyu marehemu aliko, halafu unakuja kusema sisi tulikuwa tunatekeleza matakwa ya Mwalimu, It is not fair. Mwalimu ninayemfahamu, kama angekuwepo leo angesema mzitafutie sababu za leo. Mfanye tafiti, mfanye tathmini,” alisema Profesa Baregu.

Aidha, mwanazuoni huyo alivaa viatu vya mshauri wa Rais na kueleza kile ambacho angemshauri Rais John Magufuli kuhusu mpango wa kuhamia Dodoma hivi sasa.

“Mimi ningekuwa mshauri wa Rais ningemwambia tunachoweza kufanya sasa hivi, tujiulize maswali matatu. La kwanza, kwanini tulikwama wakati ule, kama kulikuwa na sababu na vikwazo vilivyotukwamisha, tutaviondoaje. Pili tunakwenda Dodoma tuna sababu gani za leo za kutupeleka Dodoma? Tatu, kama tumeshakubalina na hayo yote, sababu ya mwishoni ile kasi yenyewe ya kuhamia,” alieleza.

Hata hivyo, Profesa Baregu alisema kuwa hapingi kuwa Makao Makuu kuhamia Dodoma, lakini anapinga hatua zilizochukuliwa kufikia maamuzi hayo hivi sasa.

Alisema kuwa ni vyema wananchi wangeshirikishwa vya kutosha na kutoa maoni yao kuhusu mpango huo kwani hata wakati wa miaka ya 19(70), enzi za Utawala wa Rais wa Kwanza, Julius Nyerere wananchi waliulizwa maoni yao.

Alisisitiza kuwa sio sahihi kwa maoni ya wananchi yaliyochukuliwa miaka ile kutumika kufanya maamuzi baada ya miaka takribani 50.

Kumuangalia mwanamke zaidi ya sekunde 14 ni kosa India, wanawake watakiwa kujifuza karate
Yametimia - Mohamed Dewji Na Uongozi Wa Simba Waafikiana