Wiki hii Chama Cha Wananchi (CUF) kilipata mtikisiko baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza uamuzi wa kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa chama hicho katika kipindi ambacho wengi hawakutegemea.

Uamuzi wa Profesa Lipumba uliitikisa pia ngome ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kuzingatia kuwa ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa wenyeviti wote wa vyama vinavyounda umoja huo.

Ukifuatilia kwa kina sababu alizozitoa Profesa Ibrahim Lipumba, ni pamoja na kuona kuwa Ukawa imepoteza muelekeo kwa kuwa imeshindwa kuzingatia tunu za taifa ikiwemo tunu ya uadilifu.

“Nimeshiriki katika vikao vingi vya Ukawa vilivyotufikisha hapa. Hata hivyo, dhamira na nafsi inanisuta kuwa katika maamuzi yetu ya Ukawa tumeshindwa kuenzi na kuzingatia Tunu za Taifa za utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi na uwajibikaji,” alisema Profesa Lipumba.

Maelezo ya Profesa Lipumba katika kipengele hicho yanaunga mkono kauli ya Kiongozi Mkuu wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe aliyesema kuwa vyama vingine vya upinzani havizingatii tunu ya uadilifu tofauti na chama chake ambacho kimeamua kuiweka tunu hiyo kwenye azimio lake la Tabora.

Zitto Kabwe aliyasema hayo alipokuwa anawahutubia wanachama wa chama hicho mjini Kigoma huku akiwapima mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa na Dk. John Magufuli na kudai kuwa hawana ubavu wa kupambana na ufisadi.

Ni kama Profesa Lipumba na Zitto Kabwe waliongea lugha moja katika vipindi tofauti katika kipengele hicho.

Ingawa Profesa Lipumba alishiriki katika kumsafisha Edward Lowassa na kumkaribisha Ukawa, alirudi kusema hadharani kuwa nafsi yake inamsuta hivyo ametafuta kile ambacho wazungu wanaita ‘peace of mind’.

Hata hivyo, muungano wa Ukawa una madhara chanya ya kidemokrasia katika taifa letu ambayo hata Zitto Kabwe alikiri kuyaona.

“Uchaguzi wa mwaka huu hata kama chama kimojawapo kitashinda hakiwezi kuunda serikali peke yake. Na kama kuna jambo ambalo tutalifanya wapinzani na wananchi wasitusamehe ni kushirikiana na CCM,” alisema Zitto Kabwe.

Zitto Adai Magufuli Sio Msafi, Amhusisha Na Ufisadi Wa Bilioni 87
Maalim Seif: Wanaotaka Kumfuata Lipumba Waende, Ukawa Iko Imara