Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), profesa Ibrahim Lipumba amekanusha taarifa kuwa yeye na Dk. Wilbroad Slaa wana mpango wa kudhoofisha upinzani kutokana na uamuzi waliouchukua katika hatua za mwisho.

Taarifa hizo zilieleza kuwa pamoja na mambo mengine, wawili hao wameamua kuudhoofisha upinzani baada ya kunyimwa nafasi ya kugombea urais kupitia Ukawa na badala yake nafasi hiyo alipewa Edward Lowassa aliyetokea CCM.

Akiongea na Azam TV, Profesa Lipumba amesema kuwa wao ndio wapinzani hasa na kuonesha jinsi walivyoumia kutokana na uamuzi wa Ukawa kumkaribisha Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea urais huku wakiacha msingi wa hoja yao ya kupata katiba mpya.

“Wapinzani ni sisi, ukisema wapinzani ni sisi… mimi nimekuwa mwenyekiti wa Chama Cha CUF toka mwaka 1999. Niliingia katika mapambano wakati kura zimeibiwa Zanzibar, tumefanya maandamano nimevunjwa mkono, nikaibiwa saa yangu na nimewekwa ndani,” alisema.

“ Sisi ndio wapinzani, wakati matukio haya yote yanatokea mheshimiwa Edward Lowassa hakuwemo katika mapambano haya, kwahiyo hauwezi kusema sisi tunavunja nguvu upinzani wakati sisi ndio vinara wa upinzani,” aliongeza.

Profesa Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) siku chache baada ya kushiriki katika kumpokea Edward Lowassa ndani ya Ukawa akidai kuwa nafsi yake inamsuta.

 

Tathmini Ya Usajili Wa Wachezaji Waliokosa Sifa
Lowassa Kuibua Mapya Urais