Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amewataka Viongozi na Watumishi katika ofisi hiyo kuzingatia weledi, nidhamu na maadili ya utumishi wa umma ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi, huku akisisitiza uwepo wa mabaraza ya wafanyakazi katika maeneo ya kazi ambayo yamekuwa ni chachu ya kuongeza ufanisi na tija kwa wafanyakazi kwa kuimarisha ushirikiano.
Ameeleza kuwa, wajibu wa kila mtumishi kufanya kazi kwa bidii na nidhamu ya hali ya juu huku akisisitiza uwepo wa mabaraza ya wafanyakazi katika maeneo ya kazi ambayo yamekuwa ni chachu ya kuongeza ufanisi na tija kwa wafanyakazi kwa kuimarisha ushirikiano.
“Ni matumaini yangu kwamba kupitia mabaraza haya ya wafanyakazi tutaweza kuimarisha mshikamano, kufanya kazi kwa umoja, hivyo tuhakikishe ushauri na mawazo yatakayotolewa na watumishi katika mabaraza itakuwa ni chachu ya kuhamasisha tija katika utekelezaji wa majukumu yetu sambamba na kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo,” Amesema Prof. Ndalichako.
Ameongeza kuwa, Ofisi hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha mwaka moja wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo shughuli mbalimbali katika sekta hiyo zimefanyiwa kazi kwa wakati.
“Tuendelee kuhakikisha maelekezo yote yanayotolewa na Rais Samia katika kukuza uchumi wa Taifa letu ili uwafikie wananchi kikamilifu yanafanyiwa kazi kwa ufanisi na wakati,” amefafanua Prof. Ndalichako
Hata hivyo Prof.Ndalichako amewataka viongozi wa TUGHE kuendelea kushirikiana na Uongozi wa ofisi hiyo pamoja na watumishi. Pia aliwasihi watumishi kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la TUGHE tawi la Ofisi hiyo Bw. Godfrey Chacha alieleza kuwa Baraza pamoja na majukumu mengine lina kazi ya kupanga mipango na kushauri viongozi na watumishi kuhusu ufanisi wa kazi na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa kuhakikisha kuwa huduma zinatolewa kwa wakati na kwa ubora unaokubalika ili kufanya kazi kwa uadilifu.