Tanzia ya Prof Haki Ngowi ambaye ni mhadhiri Chuo Kikuu cha Mzumbe,imepokelewa kwa hisia mseto huku idadi kubwa ya Watanzania wakimzungumzia jinsi alivyokuwa mtu wa watu.
Viongozi,wanadini na wananchi wa kawaida,kwa nyakati tofauti,wametumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kumzungumzia mchumi huyo.
Habari za kifo cha Profesa Ngowi zimesambaa mapema leo, ya kwamba amefariki kwenye ajali kutokana na gari aliyokuwa akisafiria kuangukiwa na kasha la mizigo (container) eneo la Chalinze mkoani Pwani leo Machi 28, 2022.
Pamoja na mchumi huyo ajali hiyo pia imetoeka na maisha ya dereva wake aliyekuwa akimwendesha kuelekea mkoani Morogoro.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram mwanaharakati Godlisten Malisa ameandika, “Dunia imempoteza mtu muhimu sana, taifa limepoteza lulu sisi marafiki zako tumepoteza mtu aliyegusa maisha yetu kwa namna ya kipekee. Kwaheri kaka mkubwa, kwaheri Profesa Ngowi. Kwaheri mwalimu.”
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Morogoro Albert Msando ameandika, “Pumzika kwa amani Profesa Ngowi, ulikuwa zaidi ya mwalimu. Ulitusimamia utafiti kwa upendo mkuu. Ulituelimisha kama rafiki zako. Ulitaka wakati wote tuwe bure kielimu na kifikra. Ulitujenga. Mzumbe na taifa limepoteza mtu muhimu sana.”
Aidha, mbunge wa Chalinze Ridhiwan Kikwete ameandika, “Sad indeed (huzuni kubwa) kumpoteza msomi na mchumi nguli. Mungu ndiye anajua sababu za kuletwa na kutwaliwa kwako. Pumzika kwa amani msomi. Mchango wako utaenziwa milele.”