Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain wameripotiwa kuwa na matumaini ya kuipiku Arsenal katika usajili wa mchezaji, Moussa Diaby, kama mbadala wa Lionel Messi.
Diaby mwenye umri wa miaka 23 anavutia timu nyingi kutokana na kiwango chake katika klabu ya Bayer Leverkusen msimu huu.
Mfaransa huyo amefunga mabao 14 na kutoa asisti 11 msimu huu na kuisaidia timu yake kushika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga.
Diaby alijiunga na kikosi cha Leverkusen akitokea PSG mwaka 2019 kwa ada ya paundi milioni 13.
Na Leverkusen sasa wanaweza kupata faida nzuri, kwa mujibu wa Evening Standard ilisema PSG wa naweza kumrejesha kwa mkataba wa pauni milioni 65.
Miamba hao wa Ligue 1 wanalenga wachezaji chipukizi wa Ufaransa wanapojiandaa kuwaachia Messi na Neymar, ambao wanakabiliwa na mustakabali usio na uhakika hapo Parc des Princes.