Washambuliaji Kylian Mbappe na Edinson Cavani hawatokua sehemu ya kikosi cha Paris St Germain, ambacho kesho jumatano kitaanza mshike mshike wa kuwania taji la Ulaya kwa kupambana na mabingwa wa kihistoria Real Madrid.

Mbappe anaendelea kusumbuliwa na maumivu ya misuli ya paja alioyapata wakati wa mchezo wa ligi ya Ufaransa mwezi uliopita dhidi ya Toulouse, huku Cavani ambaye ni raia wa Uruguay, akisumbuliwa na maumivu ya paja.

Taarifa za wawili hao kuendelea kukaa nje ya uwanja, zimethibitisha na meneja wa PSG Thomas Tuchel, na kuchapishwa kwenye tovuti ya klabu hiyo tajiri jijini Paris.

PSG pia watamkosa mshambuliaji wao kutoka nchini Brazil Neymar, ambaye anatumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu na shirikisho la soka barani Ulaya UEFA, kufuatia kumtusi mwamuzi msaidizi, wakati wa mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Manchester United, msimu uliopita.

Mbappe, Neymar na Cavani kwa pamoja waliifungia PSG mabao 11 miongoni mwa mabao 20 katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu uliopita, huku msimu huu wakitarajiwa huenda wakafunga zaidi, kutokana na misingi na malengo yaliyowekwa na uongozi wa klabu hiyo, ya kuhakikisha wanafika mbali na ikiwezekana kutwaa taji la Ulaya.

Tume ya Madini yaiwakia kampuni ya TANCOAL, yaidai 'mabilioni'
Video: JPM aibua kashfa ya ununuzi wa rada, IGP Sirro hakuna aliye salama