Mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint Germain, wamehusishwa na taarifa za kuwa mbioni kumsajili kiungo wa Arsenal ya England Matteo Guendouzi.

Klabu ya Arsenal imemuweka sokoni kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21, kwa gharama ya Pauni milioni 30, na meneja Mikael Arteta amedhamiria kumuuza Guendouzi katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye gazeti la Football London, PSG wamedhamiria kumsajili kiungo huyo, na wakati wowote wataelekea London kuanza mazungumzo ya kumrejesha nyumbani.

Guendouzi alikuzwa kisoka kwenye kituo cha vijana cha PSG kuanzia mwaka 2005 hadi 2014, na baada ya hapo alijiunga na klabu ya Lorient.

Miamba hiyo ya Ligue 1, imekua ikimfuatilia kwa ukaribu Guendouzi na imeonyesha kuridhishwa na kiwango chake, japo kwa upande wa meneja wa Arsenal, Arteta ameonekana kuwa mchezaji mwenye nidhamu mbovu uwanjani.

Guendouzi aliingia kwenye matatizo na Arteta June 20, baada ya kuonyesha utovu wa nidhamu wakati wa mchezo dhidi ya Brighton & Hove Albion, kwa kumkunja mchezaji wa klabu hiyo Neal Maupay, na kisha kumtolea maneno machafu. Katika mchezo huo Arsenal walipoteza kwa kufungwa mabao mawili kwa moja.

Mbali na tukio hilo, Guendouz alionyesha utovu mwingine wa nidhamu kwa kuandika kwenye ukurasa wake wa Twiter: “Michezo miwili, alama 6! Najivunia timu yangu… Turudi kazini @Arsenal.”

Mbali na PSG, klabu ya Valencia imejaribu kufanya mazungumzo Arsenal kuhusu usajili wa Guendouzi, lakini mambo yameonekana kuwa magumu katika makubaliano ya ada ya usajili.

FC Barcelona na mabingwa wa ligi ya Italia (Serie A) Juventus, nao wameonyesha nia ya kumsajili Guendouzi, katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

Guendouzi alisajiliwa na miamba hiyo ya kaskazini mwa London Julai 28 mwaka 2018, akitokea Lorient kwa ada ya Pauni milioni 8.

Nuru ya ushindi yaonekana Young Africans
Alphonse Areola atua Craven Cottage