Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), imewataka waajiri katika sekta za umma na binafsi kuwaondoa katika vitengo vya ununuzi na ugavi wafanyakazi wasio na sifa za kitaaluma.
Wito huo umetolewa leo Mei 16, 2022 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi mtendaji wa PSPTB, Godfrey Mbanyi baada ya kubaini uwepo wa taasisi zinazoajiri watu ambao hawajasajiliwa na Bodi hiyo kufanya shughuli za ununuzi na ugavi, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
“PSPTB inawaagiza waajiri katika sekta za umma na binafsi kuhakikisha inawaondoa watu wa ununuzi na ugavi wasio na sifa na wasiosajiliwa na bodi kama sheria inavyoelekeza,” amesema Mkurugenzi Mbanyi.
Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB amewaambia waandishi wa habari kuwa wataalam wa vitengo hivyo wanatakiwa kuhakikisha wamesajiliwa na Bodi kwa mujibu wa sheria na taratibu. Pia, amewataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma zao.
Aidha, Mbanyi amesema kwa mujibu wa muongozo wa usajili wa PSPTB na muundo wa kada zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, waajiri wanatakiwa kuhakikisha wakuu wa vitengo vya ununuzi na ugavi wana sifa ya usajili wa ngazi ya juu.
“Kuwaondoa wakuu wa vitengo vya ununuzi na ugavi wasio na sifa kunatokana na waraka namba 03 wa mwaka 2015 na tunasisitiza waajiri kuajiri watu wenye sifa kama utaratibu unavyotaka,” amesisitiza Mbanyi.
PSPTB ni miongoni mwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ikianzishwa kwa sheria namba 23 ya mwaka 2007 ikiwa na majukumu ya kupanga, kuelekeza, kuratibu na kufuatilia mahitaji ya wataalamu kwenye taaluma ya ununuzi na ugavi.