Rais wa Urusi Vladimir Putin ameamuaru taifa la Ukraine kuinua mikono au vikosi vyake viendelee kurindimisha mashambulizi nchini humo.
Kwa mujibu wa utawala wa Moscow, kusitishwa kwa uvamizi huo kutafanyika tu iwapo utawala wa Kyiv utaamuru vikosi vyake kukoma kukabiliana na Urusi pamoja na kutekeleza matakwa ya Urusi.
Kupitia kwa njia ya simu, Putin alimwambia rais wa Uturuki Tayyip Erdogan kuwa alikuwa tayari kwa mazungumzo kumaliza vita hivyo, huku Kremlin ikisema kuwa jaribio lolote la Ukraine kujiondoa katika mazungumzo hayo halitafaulu.
Vita kati ya vikosi vya Ukraine na Urusi vilizuia watu laki mbili kutoroka katika jiji la Mariupol kwa siku ya pili, ikiwa wengi wa wakazi wa jiji hilo wakiwa kwenye maficho ya ardhini.
Kwa mujibu wa mamlaka za Ukraine, vikosi vya Urusi vimekatiza usambazaji wa chakula, maji na umeme katika jiji hilo la Mariupol.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Urusi, Vikosi vya usalama vya Urusi vimewakamata zaidi ya watu 3,500 kwa kushiriki maandamano ya kushinikiza kumalizwa kwa vita kati ya Urusi na Ukraine na watu 1,700 kati ya waandamanaji hao walinaswa katika jiji la Moscow huku wengine 750 wakikamatwa jijini St Petersburg.
Hata hivyo kundi moja la uangalizi la maandamano limefutilia mbali idadi hiyo na kudai kuwa polisi nchini humo wanawazuilia zaidi ya waandamanaji 4,600 na sio 3,500 inavyoarifiwa.
Kwa mujibu wa video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na wanaharakati wa upinzani na maelfu ya waandamaji walipiga kambi katika miji ya Urusi wakikemea uvamizi wa taifa lao nchini Ukraine, wakitamka “Hatutaki vita!” na “Aibu ikupate!”