Kupitia hotuba yake kwa njia ya televisheni, Rais wa Urusi, Vladimir Putin amezionya nchi za Magharibi kwa maneno yasiyoweza kuepukika akidai kwamba jaribio la kuidhoofisha au kuishinda Urusi linaweza kuibua janga la nyuklia na kutangaza kampeni mpya ya uhamasishaji wa kuwaita takriban askari wa akiba 300,000.
Hatua hiyo, imefanya waandamanaji kote Urusi kujitokeza barabarani kuonyesha kutoidhinisha sera hiyo ambapo takriban watu 1,252 kutoka miji 38 walizuiliwa, huku shirika la kutetea haki za binadamu ambalo linafuatilia shughuli za polisi likithibitisha uwepo wa tukio hilo.
Maandamano hayo, yameharamishwa kikamilifu nchini Urusi, ambapo kabla ya wiki hii karibu watu 16,500 walikuwa wamezuiliwa kwa shughuli za kupinga vita, wakidai kuchoshwa na mapigano yasiyo na faida kwa pande zote mbili.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, Rais Biden alimkashifu Putin na kumshutumu kwa kutaka kuizima Ukraine na watu wake ili kurudisha ulimwengu nyuma kuelekea makabiliano ya nyuklia, na akaapa kusimama na Ukraine.