Rais wa Urusi, Vladimir Putin hii leo Oktoba 5, 2022 amesaini sheria inayohalalisha nchi yake kuchukua majimbo manne ya Ukraine ambayo alitangaza kuyamiliki hivi karibuni na kitendo hicho kupingwa na baadhi ya Mataifa ikiwemo la Marekani ingawa aliwashinda kwa kura yake ya turufu.
Hatua hiyo, inakuja kutokana na hati ambazo zimechapishwa katika tovuti rasmi ya serikali ya nchi hiyo, na maelezo yanaonesha kwamba, majimbo yaliyochukuliwa ni Donetsk, Lugansk, Kherson na Zaporizhzhia ambayo yamekubaliwa kuwa sehemu yao kulingana na katiba ya Shirikisho la Urusi.
Urusi, ilichukua maneo hayo baada ya kuandaa kile ilichokiita kura ya maoni, lakini iliyokosolewa na kupingwa vikali na Ukraine Pamoja na jumuiya ya kimataifa bila mafanikio.
Kusainiwa kwa sheria hiyo na Putin, kunakamilisha mchakato wake wa kuchukua kwa njia isiyo halali majimbo hayo manne ya Ukraine, huku nchi yake ikitarajia kujadiliwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatatu wiki ijayo (Oktoba 10, 2022).