Shirikisho la soka nchini Algeria limemtangaza mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo Rabah Madjer kuwa kocha mkuu, badala ya Lucas Alcaraz aliefukuzwa kazi mwanzoni mwa mwezi huu.

Madjer, mwenye umri wa miaka 58, anakua kocha wa tano kukinoa kikosi cha Algeria ndani ya miaka mitatu, na atakua na kazi kubwa ya kuiwezesha nchi hiyo kufaulu kucheza fainali za Afrika za 2019, baada ya kushindwa kufuzu fainali za kombe la dunia 2018.

Kushindwa kufikia lengo la kufuzu fainali za kombe la dunia, ilikua sababu kubwa kwa shirikisho la soka nchini Algeria kumtimua kazi Alcaraz, hali ambayo inachukuliwa kama changamoto kwa Madjer endapo atashindwa kuivusha timu kwenye fainali za Afrika za 2019.

Madjer, anakumbukwa kwa uwezo wake wa kucheza soka akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Algeria sambamba na kwenye klabu ya FC Porto ya Ureno, ambayo aliiwezesha kutwaa ubingwa wa kombe la Ulaya mwaka 1987 dhidi ya FC Bayern Munich.

Alianza kuitumikia timu ya taifa mwaka 1994, na alitangaza kustaafu mwaka 2002 baada ya kushindwa kuiwezesha Algeria kuvuka hatua ya makundi katika fainali za Afrika.

Mtihani wa kwanza kwa Madjer kama kocha mkuu wa Algeria utakua mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka 2018, ambapo kikosi chake kitapambana na Gambia.

Mwanzoni mwa mwezi ujao Madjer atakiongoza kikosi chake katika mchezo wa kukamilisha ratiba ya kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Nigeria, ambao wameshakata tiketi ya kwenda Urusi.

Rafa Benitez akataa kurithi mikoba Goodison Park
Trump akana kumtolea lugha ya dharau mke wa mwanajeshi aliyeuawa