Klabu ya Leicester City imekubali kumsajili mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Algeria Rachid Ghezzal, baada kutakiwa kutoa kiasi cha Pauni milioni 10 na uongozi wa AS Monaco ya Ufaransa.
Ghezzal alianza kufuatiliwa na uongozi wa Leicester City baada ya kuuzwa kwa mchezaji mwenzake kutoka nchini Algeria Riyad Mahrez, aliyetimkia Manchester City mwanzoni mwa mwezi uliopita.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, amesaini mkataba wa miaka minne ambao utamuweka King Power Stadium hadi mwaka 2022.
“Ni mchezaji mwenye kiwango cha hali ya juu, tunaamini atafanikisha mipango tuliojiwekea kwa msimu wa 2018/19, alisema meneja wa Foxes Claude Puel alipohojiwa na kituo cha televisheni cha klabu huyo (LCFC TV).
“Ninaufahamu ziruri uwezo wake tangu akiwa na klabu ya Lyon, akiwa na kikosi cha vijana, ninaamini mazingira ya soka la England yatampendeza na kucheza soka lenye ushindani kama ilivyokua Ufaransa.”
Ghezzal alijiunga na AS Monaco mwanzoni mwa msimu uliopita, na alifanikiwa kucheza michezo 33.