Klabu ya Manchester City inataka kurejea kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya kiungo wa Klabu ya West Ham, Lucas Paquetá.
Man City wamekubali mkataba wenye thamani ya Pauni Milioni 80 kwa kanuni kwa ajili ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 msimu wa joto, lakini hawakukamilisha uhamisho huo baada ya kubainika kuwa alikuwa akichunguzwa kwa madai ya Uvunjaji wa sheria za kamari.
Hata hivyo, ripoti za hivi punde zinaonesha Man City “wamedhamiria” kutoa ofa mpya ya kuinasa saini yake mwezi Januari 2024, kama wanaweza kupata ufafanuzi kuhusu hali yake.
Kocha Pep Guardiola anaripotiwa kumuona kama mrithi muda mrefu wa Kevin De Bruyne, ambaye anatazamiwa kumaliza mkataba wake na Man City mwaka 2025, pia amekuwa akipambana na tatizo la misuli ya paja msimu huu 2023/24.
Paqueta amesalia kuwa mchezaji muhimu wa West Ham katika kampeni ya sasa, akiwa amecheza mechi 15 katika mashindano yote kwa kikosi cha kocha David Moyes, alifunga bao la ushindi wakati wagonga nyundo hao wakiilaza Olympiacos 1-0 kwenye Ligi ya Europa Alhamisi (Novemba 09).