Klabu ya Inter Milan imethibitisha kumsajili kiungo kutoka nchini Ubelgiji Radja Nainggolan kwa mkataba wa miaka minne.
Nainggolan amejiunga na magwiji hao wa mjini Milan akitokea AS Roma, huku mkataba aliousaini utafikia kikomo Juni 2022.
Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa, usajili wa Nainggolan umeigharimu klabu hiyo kiasi cha Euro milioni 24, pamoja na kuwatoa Davide Santon na Nicolo Zaniolo kwenda AS Roma.
“Radja Nainggolan amekua mchezaji rasmi wa klabu yetu,” imeeleza taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Inter Milan.
“Kiungo huyu kutoka Ubelgiji amekubali kusaini mkataba wa miaka minne, ambao utamuwezesha kuwa nasi hadi Juni 30 mwaka 2022.
“Tunaamini usajili wake klabuni hapa, utaleta manufaa makubwa kwa msimu ujao, na lengo linalokusudiwa litakamilika kutokana na ushirikiano mzuri utakaojengeka baina ya mchezaji huyu na wachezaji wengine wa Inter Milan!”
“Uongozi wa klabu unawataka mashabiki kumpa ushirikiano mchezaji huyu, mwenye kipaji kikubwa, na ametuahidi atapambana vilivyo ili kuipa mafanikio klabu yetu.”
Kiungo huyo anaejulikana kwa jina la utani la Ninja, ana uzoefu mkubwa katika soka la Italia, baada ya kucheza michezo 250 ya ligi ya nchi hiyo (Serie A) akiwa na klabu za Piacenza, Cagliari na AS Roma.
Kwa upande wa timu yake ya taifa ya Ubelgiji, Nainggolan amecheza michezo 30 na kufunga mabao sita. Lakini hakubahatika kuwa sehemu ya kikosi kinachoshiriki fainali za kombe la dunia zinazoendelea nchini Urusi.