Kiungo kutoka nchini Ubelgiji Radja Nainggolan anatarajia kukutana na wakala wake mjini Monaco, Ufaransa kwa ajili ya mazungumzo ya kuanza harakati za kuihama klabu ya AS Roma inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Italia.
Wawili hao wanakutana huku klabu ya Inter Milan ikitajwa kuwa katika hatua nzuri ya kumsajili kiungo huyo, ambaye ameachwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ubelgiji kinachoshiriki fainali za kombe la dunia, zinazoendelea nchini Urusi.
Tayari Nainggolan ameshathibisha taarifa za kuwekwa sokoni na uongozi wa AS Roma katika kipindi hiki cha dirisha la usajili, na kama atakamilisha mpango wa kujiunga na Inter Milan huenda akauzwa kwa Euro milioni 24.
Inter milani wapo tayari kutoa kiasi hicho cha pesa sambamba na wachezaji wao Nicolò Zaniolo na Davide Santon, ambao wamejumuishwa kwenye dili hilo.
Kama atafanikisha mpango huo, Nainggolan anatarajiwa kupimwa afya siku ya jumanne juma lijalo, na atasaini mkataba wa miaka minne wa kuitumikia klabu ya Inter Milan.