Kiongozi wa Umoja wa watu waliokuwa wakimuunga mkono Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kwenye harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hemed Ali ametoa ya moyoni kuhusu uamuzi wa mwanasiasa huyo kurejea kwenye chama chake hicho cha zamani.
Lowassa ambaye mwaka 2015 alihama CCM na kujiunga na Chadema ambapo alipewa nafasi ya kugombea Urais, wiki iliyopita alitangaza kurejea tena CCM katika hatua aliyoielezea kuwa ‘amerudi nyumbani’.
Hemed Ali ambaye alikuwa akiratibu uungwaji mkono wa Lowassa enzi hizo kupitia makundi ya 4U Movements na Friends of Lowassa, ametoa waraka wake akielezea jinsi ambavyo wamepokea taarifa hizo.
Ali ameeleza kuwa endapo Lowassa angemueleza na kumpa dakika moja amshauri, basi angemshauri astaafu siasa.
“Uamuzi huu ni haki yake ya kidemokrasia, hajanihusisha kwa hatua yoyote ile na haikuwa lazima pia kunihusisha. Lakini laiti angenipa dakika moja kabla hajahama ningemkumbusha ya 2015,” Ali ameandika.
Amedai kuwa angemkumbusha jinsi ambavyo alikutwa na misukosuko ya kusemwa, kejeli pamoja na dhihaka kutoka kwa baadhi ya watu ndani ya CCM.
“Pia ningemkumbusha heshima ya Watanzania zaidi ya Milioni 6 waliotupa kura ndani ya Chadema waliotupigia kura kwa imani kubwa, na miongoni mwao wapo waliosimama pamoja kumpigania,” aliongeza.
Aidha, alieleza kuwa angemshauri asubiri Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe atoke mahabusu, azungumze naye kabla ya kuchukua uamuzi huo lakini kwa sasa hayo yote hayawezekani kwani tayari ameshatekeleza uamuzi wake.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt. Vincent Mshinji ameiambia Mwananchi kuwa Lowassa aliondoka bila kumwambia mtu yeyote.
Hata hivyo, Dkt. Mashinji amesema kuwa hawakushangazwa na uamuzi huo kwani ni jambo la kawaida kwa wanasiasa kuchukua uamuzi kama huo.