Mwenyekiti wa zamani wa Simba SC Ismail Aden Rage ameipongeza Klabu ya Young Africans kwa kufanikiwa ndani na nje ya Uwanja, baada ya kupitia kipindi kigumu kwa miaka ya hivi karibuni.
Young Africans ilirejesha heshima ya Ubingwa msimu uliopita, wakiutwaa kutoka kwa Watani zao Jadi Simba SC waliotawala Soka la Bongo kwa misimu minne mfululizo.
Rage amesema kujitambua, upendo na mshikamano vimekua sababu kubwa ya mabadiliko ndani ya Young Africans, ambayo inaendelea kutamba katika Soka la Bongo, huku wakitinga hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
“Wanastahili hiki kinachoendelea kwa sababu wana viongozi wa mpira, umoja baina ya wao kwa wao, kitu ambacho sio rahisi kukiona kwenye klabu nyingine kwa sasa,”
“Unapokosea ndio njia sahihi ya kujirekebisha, Young Africans ilipitia misukosuko ila iliichukulia kama Fursa ya kuwajenga na kutatua pale walipokosea, ndio maana tunaona leo wamefanikiwa.” amesema Rage
Kuhusu Mbio za Ubingwa Rage amesema licha ya kasi ya Young Africans ila bado ni mapema kuzungumzia hilo, kwani Azam FC na Simba SC nazo zinaonyesha kuwa tayari kuupambania msimu huu.
“Ukiwaangalia na washindani wengine utagundua wametulia na wanapambana ili kusaka ubingwa msimu huu, kwa mfano Azam FC na Simba SC, naamini bado ni mapema mno kusema Bingwa atakuwa nani.”
“Young Africans anatajwa sana kwa sababu yupo kileleni kwa sasa, lakini ukweli ni kwamba soka lina tabia mbaya sana ya kubadilika badilika, hivyo kwa nani atakuwa bingwa msimu huu ninaomba niwe kimya na mnitafute baadae.” amesema Rage
Young Africans inangoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 32 sawa na Azam FC inayoshika nafasi ya pili, huku Simba SC yenye alama 31 ikishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23.