Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC Ismail Aden Rage, amesema amebahatika kufanya kikao na Benchi la Ufundi la timu hiyo pamoja na wachezaji na kuwapa mbinu ambayo itawasaidia kwenye michezo inayofuata ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Rage ambaye alikuwa nchini Morocco kushuhudia mchezo wa kukamilisha hatua ya makundi kati ya timu hiyo na Raja Casablanca iliyoshinda 3-1, amesema kitakachowasaidia kwenye michezo inayofuata si kukaba njia tena bali ni kwa staili ya mtu kwa mtu ‘Police Marking’, ambayo anaona itawabeba zaidi kwenye michezo inayofuata.

“Mpira ulipokwisha nilikwenda kutoa ushauri wangu, nikaongea na Makocha na Baadhi ya wachezaji na niliwaambia wajitahidi kwenye michezo inayokuja kufanya aina ya ulinzi inayoitwa mtu kwa mtu, ‘Police Marking’, badala ya kukaba njia, yaani wakati mnashambuliwa mnahakikisha wale wapinzani wenu hawawi peke yao, hamkai nao mbali, ili wasijiandae na kufanya wanachokitaka wakati wanapokuwa na mpira, mkiwa nao mbali, inakuwa ni hatari, lakini mkiwa nao karibu wakigusa tu mpira mnawadhibiti, nina imani kabisa kuwa watafanya jitihada hizo,” amesema Rage.

Kuhusu mchezo wa mwisho wa Kundi C dhidi ya Raja Casablanca Rage amesema Simba SC ilicheza vizuri lakini kulikuwa na matatizo upande wa ulinzi ndiyo yaliyofanya wapoteze.

“Simba wamecheza vizuri, lakini wamepoteza mchezo, kwenye soka hili lipo, unaweza kucheza vizuri, lakini ukafungwa, matatizo makubwa yalikuwa ni kwenye upande wa ulinzi, ambapo walifanya makosa hayo hayo na timu hii tulipocheza Dar es Salaam na ndiyo maana nikawapa hiyo mbinu, lakini mimi binafsi nilishtuka sana nilivyoona kiwango kile cha Simba, kilikuwa kizuri sana nikielewa hali halisi ya wachezaji wetu tuliokuwa nao, tunakwenda Robo Fainali, lakini kikubwa zaidi ni kwamba katika mashindano mengine makubwa yanayokuja tunatakiwa tujiimarishe kwenye sehemu ya ulinzi, viungo wakabaji na safu ya ushambuliaji iongezwe nguvu,” ameshauri Rage.

Kikosi cha Simba kilirejea nchini jana Jumapili (April 02) na kinasubiri keshokutwa, Jumatano (April 05) Droo ya michuano hiyo itakapopangwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, ili kujua itacheza na timu gani kwenye hatua ya Robo Fainali ambapo itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa na kwenda kumalizia ugenini.

Baada matokeo ya makundi yote kukamilika juzi, Simba itacheza na timu kati ya Wydad Casablanca ya Morocco ambao ni vinara wa Kundi A, Mamelodi Suudowns ya Afrika ya Kusini ikiliongoza Kundi B au Esperance ya Tunisia, ambao wapo kileleni kwenye Kundi D.

Nabi: Nilioteshwa Farid Mussa kuifunga TP Mazembe
Dakika 270 za moto Azam FC