Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba SC Ismail Aden Rage ameutaka uongozi wa klabu hiyo kulipa FIFA, faini ya Dola za kimarekani Laki Moja na Thelathini (150,000), sawa na Shilingi za Tanzania milioni Mia Tatu (300,000,000).
Simba wametakia kulipa kiasi hicho cha pesa kama faini, baada ya kubainika walimsajili kimakosa mshambuliaji Shiza kichuya mapema mwaka huu, akitokea kwenye klabu ya Pharco ya Misri.
Shirikisho la soka duniani (FIFA), lilitangaza adhabu ya kumfungia miezi sita mshambuliaji huyo wa klabu ya Namungo FC, baada ya kusikiliza malalamiko yaliyowasilishwa na klabu yake ya zamani.
Kufuatia hatua hiyo Rage amewataka viongozi wa Simba SC kutii adhabu hiyo, na amewatak washukuru kwa maamuzi yaliochukuliwa dhidi.
Amesema kulikua na hatari ya klabu hiyo inayomiliki ubingwa wa Tanznaia bara kwa misimu mitatu mfululizo kupokwa alama (Point), ambazo zilipatikana kwenye michezo waliyomchezesha Kichuya msimu uliopita.
“Hata hivyo Simba SC wanatakiwa washukuru kwa kuwa wamepigwa faini tu, nadhani hii ni kwa sababu msimu ulishapita ila ingekuwa tofauti sana, na ilibidi wapokwe point za michezo yote aliyocheza Kichuya na ndio maana hata Namungo wakazuiliwa kwa miezi 6 kumtumia.” Amesema Rage.
Katika hatua nyingine mdau huyo wa soka la Bongo ameilaumu klabu ya Simba kwa kushindwa kufanya mambo kwa weledi, na kujikuta wakijiingiza kwenye matatizo kama ya kumsajili mchezaji aliekua na mkataba na klabu nyingine.
“Hii inatokana na kutokuwa na watu makini ndani ya klabu, huwezi kufanya kosa kama hili kama una viongozi wenye kujitambua. Hata hivyo viongozi wangu watambue katika hili hakuna nafasi ya kukata rufaa, zaidi ya kulipa pesa hiyo.” Aliongeza Rage.
Kichuya alijiunga na Klabu ya Pharco ya Misri msimu wa 2018 akitokea Simba SC, na alisepa kimyakimya kutokana na kukosa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza, ambapo alicheza jumla ya michezo mitatu pekee.
Alirejea Simba msimu wa 2019/20 ambapo alisaini dili la miezi sita.
Mwanzoni mwa msimu huu mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro alisajiliwa na Namungo FC, na tayari alishaanza kufanya vyema, ambapo kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Rabita ya Sudan Kusini uliochezwa Uwanja wa Azam Complex alitupia bao moja wakati timu yake ya ikishinda mabao matatu kwa sifuri.
Pia Uwanja wa Mkapa wakati timu yake ikilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Young Africans alisababisha penati moja iliyookolewa na kipa Metacha Mnata.