Aliyewahi kuwa katibu mkuu wa chama cha soka nchini FAT kwa sasa shirikisho (TFF) Ismail Aden Rage, amependekeza klabu ya Simba ikabidhiwe ubingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu huu wa 2019/20.

Rage ambaye pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo ya MSimbazi, amesema endapo hali ya janga la maambukizi ya virusi vya Corona litaendelea kutishia kurejea kwa ligi kuu, TFF wanapaswa kuwatazama Simba SC, ambao hadi ligi inasimamishwa walikua kileleni kwa kufikisha alama 71.

Rage amesema dhumuni lake ni kuona ligi inaendelea kama matarajio ya wengi ili kumpata bingwa kwa kufuatwa kanuni ya kumalizwa kwa michezo yote 38 kwa kila timu shiriki, lakini kama itashindikana njia mbadala ya kumpa ubingwa Simba inapaswa kuchukuliwa kama ilivyofanywa nchini Ubelgiji.

“Kama hali itaendelea hivi kuhusu Corona kwenye taratibu za FIFA, hali kama hii, hili gonjwa lililotokea hakuna mwanadamu aliyetegemea na ni janga la kimataifa, ni vyema tukafanya kama walivyo fanya Ubelgiji”

“Ligi imesimamishwa aliye kuwa anaongoza anaongoza aliyekuwa anashuka daraja anashuka kama hali itarudi kuwa sawa tunaweza kuendelea na ligi.”

Hata hivyo rage akewashauri TFF kufuata utaratibu wa kuwasiliana na shirikisho la soka barani Afrika CAF, ili kuwafahamisha kuhusu ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao.

Kama hiyo haitoshi Rage, akatupa dongo kwa Young Aficans kwa kuwaambia hawana chao msimu huu, endapo Simba SC na Azam FC wataiwakilisha nchi msimu ujao, na badala yake wajiandae kucheza michuano ya kombe la Mbuzi (Mbuzi Cup).

“TFF wawasiliane na CAF kujua ligi ya mabingwa na kombe la shirikisho barani Afrika wanaanza lini”

“Mimi nashauri Simba SC iwakilishe klabu bingwa na Azam FC iwakilishe kombe la shirikisho na Young Africans iwakilishe Mbuzi Cup”- maneno ya Aden Rage mwanachama wa klabu ya Simba SC.

Ligi Kuu imesimama huku Simba SC wakiwa wanaongoza kwa alama zao 71, wakifuatiwa na Azam FC alama 54 baada ya wote kucheza michezo 28, wakati vigogo Young Africans ni wa tatu kwa alama zao 51 za michezo 27 na Namungo wa nne wakiwa na alama 50 za michezo 28.

Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa alama zake 15 za michezo 29, nyuma ya Mbao FC wenye alama 22 za michezo 28, Alliance FC alama 29, michezo 29, Mbeya City alama 30 michezo 29 na Ndanda FC alama 31 michezo 29.

 

Chipsi, vinywaji vyenye sukari marufuku Simba SC
Lema: Serikali itoe nyumba bure wanaohudumia wagonjwa Covid 19