Mwenyekiti wa zamani wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC Ismail Aden Rage amesema uongozi wa Klabu ya Young Africans kuendelea kung’ang’ania kesi ya Morrison, ambayo wanadai wameifikisha kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) haitawasaidia kitu.
Rage ametoa ushauri huo kwa viongozi wa Young Africans, baada ya Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Fredrick Mwakalebela kutoa taarifa za maendeleo ya kesi ya Morisson alipozungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya mwishoni mwa juma lililopita.
Rage amesema Young Africans wanapaswa kuendelea na mambo mengine ya kimaendeleo ndani ya klabu yao, na kuachana kabisa na suala la kiungo huyo kutoka nchini Ghana, ambalo amedai litawapotezea muda.
Amesema hawawezi kupata chochote kile kupitia kesi hiyo, ambayo tayari imeshatolewa hukumu la Shirikisho la soka nchini TFF kupitia kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji chini ya mwenyekti wake Elias Mwanjala.
Hata hivyo amewataka viongozi wa Young Africans kuionesha hadharani barua wanayodai wameipata kutoka CAS, ambayo inawathibitishia kesi ya Morisson imepokelewa na kupangiwa hakimu wa kuisikiliza.
Rage akaenda mbali zaidi kwa kusema, hakuna sheria yoyote ya CAS, inayotaka mshitaki na mshitakiwa walipe pesa ili kesi yao isikilizwe katika mahakama hiyo.
“Kama viongozi wa klabu ya Young Africans wana barua kutoka CAS waioneshe hadharani, wasilete ujanja ujanja na kuwadanganya wadau wa mpira wa miguu wa nchi hii.” Rage kasema.
“Haiwezekani kila siku anajitokeza kiongozi mmoja na kudai suala la Morisson lipo CAS, halafu hatuoneshwi uthibitisho wowote kutoka kwenye mahakama hiyo ya kimataifa, mimi ninawashauri hawa wenzangu waachane na hili, waangalie mambo mengine ya kufanya.” Ameongeza Rage.
Morrison ambaye aliitumikia Young Africans kwa takribani miezi sita msimu uliopita, alijiunga na Simba SC msimu huu 2020/21 ambapo usajili wake ulileta mvutano mkubwa kiasi cha kufikishana TFF, na baadae alishinda kesi iliyothibitisha yupo huru kujiunga na timu yoyote baada ya kubaini mapungufu kwenye mkataba wake.