Aliyewahi kuwa mwenyekiti wa klabu ya Simba SC Ismail Aden Rage ameibuka na kudai kumeshangazwa kuona Young Africans wanaanika hadharani madai ya uhalali wa mkataba kati ya kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison, na waajiri wake wa sasa.

Juma lililopita Makamu Mwenyekiti Fredrick Mwakalebela akiwa na Afisa habari wa Young Africans Hassan Bumbuli, walizungumza na waandishi wa habari na kuonyesha mkataba unaodaiwa kuwa wa Morrison na klabu ya Simba SC, ambao walidai una mapungufu.

Rage ambaye pia aliwahi kuwa katibu mkuu wa Chama cha soka Tanzania (FAT) ambacho kwa sasa ni Shirikisho la soka Tanzania (TFF), amesema ameshangazwa na kusikitishwa na madai hayo.

Amesema Mwakalebela ambaye aliwahi kuwa Katibu mkuu wa TFF anapaswa kuweka wazi kila kitu, kwani mkataba wa pande mbili uliosainiwa kisheria hauwezi kuingiliwa na mtu mwingine wa kati, kama una mapungufu ya aina yeyote.

“Nimeshangaa na kusikitika madai haya yametolewa na Yanga chini ya Mwakalebela ambaye alikuwa kiongozi wa TFF aweke wazi kila kitu, kisheria mkataba wa watu wawili hauwezi kuingiliwa na mtu mwingine kati kama una mapungufu ya aina yeyote wanaotakiwa kulalamika ni Simba ama mchezaji mwenyewe Morrison” Amesema Rage

Hata Hivyo Rage amewataka viongozi wa Simba SC kuwafungulia kesi viongozi Young Africans, kupitia taarifa zilizotolewa na Makamu mwenyekiti wao Fredrick Mwakalebela, kwa kuhoji ni wapi walipozipata nyaraka ambazo ni siri kati ya mwajiri na mwajiriwa.

“Simba SC wanaweza kuwashitaki, yeye amepataje nyaraka za mkataba ambao ni siri ya watu wawili, sheria za CAF na FIFA kuna muda wa vipingamizi je kipindi hicho mbona walikaa kimya, kuna kipengele cha mkataba kinasema kuwa ‘Voidable Contract’ ni mkataba uliokamili, kama kuna mapungufu yule mmoja wapo anatakiwa alalamike”

“Hivyo, kinachotakiwa wao wenyewe wakubaliane kuurekebisha na inaruhusiwa na mchezaji anaendelea kuitumikia timu yake na iwapo hakutakuwa na makubaliano baina ya pande hizo mbili basi mkataba unaweza kuvunjika” Rage amesema.

Usajili wa Morrison kutoka Young Africans kuibukia Simba SC umekuwa na sarakasi nyingi tangu awali ambapo mwanzo kulikuwa na mvutano mkubwa kati ya mchezaji na mabosi wake wa Young Africans.

Young Africans walikuwa wakieleza kuwa mchezaji huyo ana dili la miaka miwili huku mchezaji akieleza kuwa ana mkataba wa miezi sita na umemalizika.

Utata huo ulifanya suala hilo kutinga makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambapo kesi yake iliskilizwa kwa muda wa siku tatu mfululizo na hukumu ilitolewa kwamba Morrison ni mchezaji huru kwa kuwa mkataba wake na Young Africans ulikuwa na mapungufu.

Kwa sasa limeibuka tena sakata hili ambalo nalo linaeleza kuwa bado Morrison mkataba wake ndani ya Simba una mapungufu muda ambao dirisha la usajili limefungwa na mchezaji huyo akiwa ameshacheza michezo kadhaa ndani ya Simba SC.

Pochettino kurithi mikoba Old Trafford
Forbes: Sofía Vergara muigizaji wa kike alieingiza pesa zaidi 2020